Swali: Mimi ni kijana mwenye msimamo wa dini na shukurani zote njema zinarudi kwa Allaah. Lakini hata hivyo nasumbuliwa na kushindwa kwa hali ya juu na nahisi kama kwamba macho ya watu wananichunga kwa njia ya kunidharau na kunicheza shere. Kwa sababu kanzu yangu ni fupi na utu wangu ni wa mtu wa dini. Ni zipi nasaha zako kwangu? Ni zipi nasaha zako kwa wale ambao wanawakejeli watu kama hao?

Jibu: Kitu cha kwanza mtu anatakiwa kuwa ni mwenye nguvu juu ya dini yake na ni mwenye kujitukuza nayo. Midhali ni mwenye kushikamana barabara na dini ya Allaah ipasavyo basi asimjali yeyote. Atambue kuwa hakuna mtu yeyote aliyesalimika. Mpaka Mola wa walimwengu (Jalla wa ´Alaa) alikadhibishwa na wanadamu na wakamtukana. Wamesema kuwa Allaah hawezi kumrudisha mfu. Haya ni makadhibisho. Wamesema kuwa ana mtoto. Haya ni matusi. Je, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisalimika kutokamana na watu? Hapana, si yeye wala Mitume wengine. Kila mtu ambaye ni muumini atakuwa na maadui katika wahalifu. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا مِّنَ الْمُجْرِمِينَ

“Na hivyo ndivyo Tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wahalifu.”[1]

Midhali uko juu ya haki basi jitukuze kwa haki uliyomo:

وَلِلَّـهِ الْعِزَّةُ وَلِرَسُولِهِ وَلِلْمُؤْمِنِينَ

“Na hali utukufu ni wa Allaah na wa Mtume Wake na wa waumini.”[2]

Hata kama shaytwaan atakushawishi kuwa watu wanakutweza, mshukuru Allaah na ujiambie mwenyewe kwamba kama wananitweza kwa ajili ya dini yangu basi mimi niko juu yao katika dini hii.

Kuhusiana na kanzu fupi, kanzu fupi sio mizani. Mizani ni tabia na kufuata Sunnah. Inapokuja katika kanzu itambulike kuwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) kanzu zao zilikuwa ni zenye kufika mpaka kwenye muundi. Bali Hadiyth zinafahamisha juu ya kufaa kuvaa kanzu mpaka kwenye muundi. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakupanga adhabu isipokuwa tu juu ya kile chenye kushuka chini ya kongo mbili za miguu. Midhali jambo ni lenye wasaa namna hii na mimi naona watu wanakimbia mbali na kanzu yenye kufika nusu ya muundi au hawakubali kutoka kwa mtu huyu nasaha… baadhi ya watu – naomba ulinzi kutoka kwa Allaah – hawakubali nasaha kutoka kwa yule ambaye kanzu yake inafika nusu ya muundi. Midhali jambo ni lenye wasaa namna hii basi najizuia na watu kutokamana na heshima zao na naburudika na yale aliyohalalisha Allaah. Huenda yule mwenye kushindwa ubora akawa ndiye mbora zaidi.

Ama kuhusu wale wanaowachukia watu hawa au wanawachezea shere kwa sababu ya mavazi yao, hapa tutatazama kama wanachokusudia ni yale wanayoyafanya au wanawachukia wale watu tu? Ikiwa wanachochukia ni ile haki wanayofanya, basi hapa kuna khatari ya jambo hili kuwa ni kuritadi kutoka nje ya dini ya Uislamu. Ikiwa wanawachukia wao kama wao, basi huku sio kuritadi. Lakini pamoja na hivyo ni lazima kwao kuzisubirisha nafsi zao. Nitawapigia mfano: Endapo kutakuwa na mtu ambaye watu wanamwamini na kumpenda ambaye ameifanya kanzu yake ni yenye kufika nusu muundi na mwingine si mwenye kutajwa na ni mwenye kugharimika ambapo ameifanya kanzu yake ni yenye kufika nusu ya muundi, watu watawatazama vipi? Atatazamwa zaidi yule wa kwanza kuliko wa pili na huenda pia wakamuigiliza. Kwa ajili hiyo mtu anatakiwa kutambua hadhi ya nafsi yake kati ya watu. Midhali jambo ni lenye wasaa basi asijikalifishe nafsi yake kisichokuwa cha lazima. Aidha kunafanya watu kumkimbia na kutokukubali nasaha zake juu yao.

[1] 25:31

[2] 63:05

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (68) http://binothaimeen.net/content/1531
  • Imechapishwa: 16/07/2020