Sharti ili mtu aweze kuwanukuu wanachuoni na vitabu vyao

Swali: Unajua kuwa waislamu wengi katika miji ya makafiri hawafahamu kiarabu. Katika kijiji chetu kwa mfano kuna ndugu anayewafanyia tarjama vitabu vyepesi vya wanachuoni ndugu zake kama vile ”Sharh Thalaathat-il-Usuwl” ya Shaykh Ibn ´Uthaymiyn na vyenginevyo. Akafanyiwa upinzani kwamba ni lazima kwanza afanyiwa mapendekezo maalum kutoka kwa mmoja katika wanachuoni wakubwa Salafiyyuun Saudi Arabia. Unasemaje juu ya jambo hilo?

Jibu: Yule anayejifunza kitu katika elimu na Fiqh ya Kiislamu na akakimairi, basi afanye hivo. Bali analipwa ujira akikifundisha. Haishurutishwi afanyiwe mapendekezo. Kinachotakiwa kuchunguzwa ni kitu gani anawafunza watu. Ikiwa anawafunza mambo ya sawa katika hukumu za Shari´ah kwa dalili zake, basi hilo ndilo linalotakikana. Haikuwekwa sharti apendekezwe na Shaykh.

Akikosea basi ni lazima awepo mtu wa kusahihisha kosa hilo. Kama anakosea basi haifai akawafunza watu kitu ambacho si cha sawa. Mambo ni hivyo kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Fikisheni kutoka kwangu ijapo Aayah.”

Hiyo ni dalili inayofahamisha kwamba ambaye amebeba kitu kidogo katika elimu ambacho watu wanakihitajia, basi analazimisha kukifikisha. Haijuzu kwa yeyote kumzuia muda wa kuwa hawapotoshi watu na hazungumzi juu ya Allaah pasi na elimu, anajibu pasi na elimu na anasimika kanuni pasi na elimu. Mtu kama huyu haijuzu kwake kufunza na wala haijuzu kumnyamazia. Anatakiwa kunasihiwa kwanza asome mpaka awe na kitu katika elimu ndio baadaye awafunze watu. Kwa hivyo asizuie akiwa ni mwenye kupatia. Na wala asikubaliwe akiwa ni mwenye kukosea.

Swali: Akiwa ni mwenye kufanyia tarjama maneno ya wanachuoni pasi na kuongeza wala kupunguza?

Jibu: Kama anayafikisha maneno ya wanachuoni kama yalivyo kweli, basi hakuna neno. Hivo ndivo wanavofanya wanafunzi. Wananukuu kutoka kwa wanachuoni wao na wale wanachuoni wa hapo kale ambao wametunga tungo na vitabu katika Sunnah. Awanukuu kiuaminifu. Hata hivyo ni vyema kwake akafahamu kile anachokinakili. Akiulizwa basi anaweza kupambanua suala hilo kwa hukumu ya Kishari´ah na masuala ya kidini ili asije kutumbukia kwenye kosa. Ni lazima kwa mtu afahamu kile anachokinukuu. Kwani kuna khatari mtu akanakili kitu ambacho kimepotoshwa, kimeandikwa kimakosa au makosa kabisa na matokeo yake wasikilizaji wakapatwa na madhara. Kwa hiyo ni lazima kufahamu pia.

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.al-amen.com/vb/showthread.php/7410
  • Imechapishwa: 18/01/2021