Sharti ili asali iwe ni dawa yenye kunufaisha

243- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah amesema kweli na tumbo la nduguyo limesema uongo.”

Ameipokea Muslim (07/26) kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy ambaye amesimulia:

“Kuna bwana mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akasema: “Ndugu yangu tumbo lake linamvuruga.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Mnyweshe asali.” Akafanya hivo. Kisha akaja tena na kusema: “Nimempa asali, lakini limezidi kumvuruga zaidi.” Akamwambia vivyo hivyo mara tatu. Alipokuja mara ya nne akamwambia: “Mnyweshe asali.” Bwana yule akasema: “Nimemnywesha na halikuzidi isipokuwa kumvuruga zaidi.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

 “Allaah amesema kweli na tumbo la nduguyo limesema uongo.”

Baada ya hapo akamnywesha asali na akapona. Allaaah Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “Allaah amesema kweli na tumbo la nduguyo limesema uongo” yanashuhudia manufaa ya dawa hii na kwamba kubaki kwa maradhi hakutokani na upungufu wa dawa hii yenyewe kama yenyewe. Lakini ni kutokana na wongo wa tumbo na kukithiri kwa nyenzo mbaya ndani yake. Kutokana na kwamba tumbo limekithiri nyenzo mbaya ndani yake ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwamrisha akariri dawa ileile.

Tiba ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) sio kama tiba ya madaktari. Tiba ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni yenye yakini, ya kukata shauri kabisa na ya kiungu ambayo inatokana na Wahy, mwanga wa kinabii na akili timilifu. Tiba za wengine ni zenye kutokana na kukisia, kudhania na uzoefu. Si wagonjwa wengi wanaopinga kutofanya kazi tiba ya kinabii. Ambaye ananufaika nayo ni yule ambaye anaipokea kwa kuikubali, akaamini kuwa inaponya na kuiamini na kuinyenyekea kikamilifu.

Qur-aan hii ambayo ni ponyo kwa yale yaliyomo kifuani. Lakini isipoaminiwa haitoponya yale yaliyomo kifuani. Bali haiwazidishii wanafiki isipokuwa uchafu juu ya uchafu na maradhi juu ya maradhi.

Ni vipi msimamo wa tiba za wale wazima juu yake? Tiba ya kinabii haiendani isipokuwa juu ya ile miili ilio mizuri, kama ambavo ponyo ya Qur-aan haiendani isipokuwa na zile roho nzuri na nyoyo zilizo hai. Upuuzaji wa watu kutokamana na tiba ya kinabii ni kama upuuzaji wao juu ya kujitibu kwa Qur-aan ambayo ndio shifaa yenye kunufaisha kikweli. Hayo si kwa sababu ya upungufu kwenye dawa yenyewe, lakini ni yale maumbile yenyewe ndio mabaya, kuharibika kwa mahala na kutoikubali.”[1]

[1] Zaad-ul-Ma´aad (3/98).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (1/1/489)
  • Imechapishwa: 18/04/2020