Salafiyyuun wanampenda Mtume (صلى الله عليه وسلم)

Swali: Katika vyombo vya mawasiliano kunaenezwa ujumbe unaosema:

“Ndio, tunasherehekea mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kuwa sherehe inaabiria kufurahika naye, jambo ambalo linatakikana katika Qur-aan na Sunnah na hukumu yake ni yenye kunyamaziwa.”

Vipi tutaraddi maneno haya?

Jibu: Haya ni maneno batili. Huyu anaeneza Bid´ah kwa maneno kama haya ya batili. Haijuzu kufanya hivi. Sisi tunampenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni mpendwa zaidi kwetu kuliko nafsi zetu, watoto wetu, wazazi wetu na watu wote. Hivyo ndivyo alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hatoamini mmoja wetu mpaka mimi niwe ni mpendwa zaidi kwake kuliko mtoto wake, mzazi wake na watu wote.”

´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) aliposikia hivo akamwambia: “Ee Mtume wa Allaah! Wewe ni mpendwa zaidi kwangu kuliko kila kitu isipokuwa tu nafsi yangu.” Akasema: “Hapana, ee ´Umar! Mpaka mimi niwe ni mpendwa zaidi kwako kuliko hata nafsi yako.” Baada ya hapo ´Umar akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Naapa kwa Allaah ya kwamba! Hivi sasa wewe ni mpendwa zaidi kwangu kuliko hata nafsi yangu.” Akasema: “Hivi sasa, ee ´Umar [ndiye umekuwa na imani kamilifu].”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)  ni mpendwa zaidi kwetu kuliko nafsi zetu. Kumpenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)  ni jambo la wajibu kwetu baada ya kumpenda Allaah (´Azza wa Jall). Lakini hata hivyo hatufanyi Bid´ah na kusema kuwa ndio kumpenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anachukia Bid´ah hizi. Vipi tutamuasi? Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametukataza Bid´ah. Vipi tutamuasi na kudai kuwa tunampenda? Unampenda ilihali unamuasi? Mapenzi yako wapi?

Unamuasi Muumba
na huku unadai wampenda?

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Ighaathat-il-Lahfaan (63) http://alfawzan.af.org.sa/node/16495
  • Imechapishwa: 26/08/2017