Safarini kunaachwa kuswaliwa swalah za Sunnah zote?

Swali: Mtu akiwa Makkah na akawa anaswali katika msikiti Mtakatifu ilihali ni msafiri. Je, bora kwake ni kuswali swalah za Rawaatib au bora ni kuziacha? Akiziacha anaandikiwa swalah laki moja au anaandikiwa swalah moja?

Jibu: Kwanza muuliza anasema kuwa msafiri anaacha Rawaatib. Uhakika wa mambo ni kwamba haachi Rawaatib. Anachoacha ni Raatibah ya Dhuhr, Maghrib na ya ´Ishaa. Kwa msemo mwingine ni kwamba msafiri haachi katika swalah za Nawaafil isipokuwa hizi tatu peke yake. Zindukeni juu ya hilo. Kwa sababu kuna baadhi ya watu wanasema kuwa ni katika Sunnah mtu anapokuwa safarini kuacha kuswali swalah za Sunnah. Matokeo yake utamuona haswali swalah ya Dhuhaa wala haswali swalah za usiku. Yote haya ni kujengea juu ya uelewa huu ambao wamefahamu, jambo ambalo ni la makosa. Tambua, ee  ndugu yangu, ya kwamba msafiri anaswali swalah za Sunnah zote isipokuwa hizi tatu tu. Nazo ni Sunnah ya Dhuhr, ya Maghrib na ya ´Ishaa.

Ama mtu akiwa Makkah, bora kwake ni yeye asiswali swalah za Sunnah hizi tatu kama tulivyosema. Lakini hata hivyo atumie fursa ya kuswali katika msikiti Mtakatifu kwa kunuia kwamba ni Sunnah zisizofungamana (نفل مطلق) na sio Raatibah. Sunnah zisizofungamana inafaa kwa msafiri kuswali kiasi atakavyo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (37) http://binothaimeen.net/content/840
  • Imechapishwa: 30/03/2018