Sababu zinazopelekea watu waliomo ndani ya makaburi kuadhibiwa. Sababu hizo zimegawanyika sehemu mbili:

1- Kwa jumla.

2- Kwa ufafanuzi.

Kuhusiana na za jumla watu waliyomo ndani ya makaburi wanaadhibiwa kwa kutokumjua kwao Allaah (Ta´ala), kupuuzia maamrisho Yake na kufanya madhambi. Allaah haiadhibu roho iliyomjua, ikampenda, ikatekeleza maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake. Hakika adhabu ya kaburi na Aakhirah inatokana na khasira za Allaah kwa mja. Yule ambaye Allaah atamkasirikia katika dunia hii na akafa katika aliyomo pasina kutubia, atapata adhabu ya kaburini kwa kiasi na jinsi Allaah alivyomkasirikia. Kuna waliokasirikiwa kidogo na kuna waliokasirikiwa sana, msadikishaji na mkadhibishaji.

Sababu ya ufafanuzi ni kama ilivyopokelewa katika maandiko miongoni mwa uvumi, kutojichunga na mkojo, kula nyama za watu, kuswali pasina twahara, atayempitia mdhulumiwa na asimnusuru, atakayesema uongo wenye kufikia upeo wa unafiki, mwenye kusoma Qur-aan usiku kucha na kutoitendea kazi mchana, yule ambaye ni mzito inapokuja katika swalah, asiyeitolea mali yake zakaah, mzinifu, mwenye kuzua fitina kwa maneno na mahubirio, mwenye kuchukua kitu kabla ya kugawa ngawira na kula ribaa.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (02/617-618)
  • Imechapishwa: 19/05/2020