Sababu Ya Syria Kutokuwa Jihaad


Swali: Hivi sasa niko naandika Ahl-us-Sunnah wanachinjwa na heshima zao zinavunjwa huko Syria ilihali nyinyi mmekaa tu kwenye mizunguko ya kielimu. Ni kipi kinachotakiwa kupewa kipaumbele?

Jibu: Unataka mimi nifanye nini? Mimi nitakueleza kile kinachotakiwa kupewa kipaumbele. Kitu cha kwanza nakwambia kuwa Allaah ndiye anayejua yale yaliyomo ndani ya mioyo yetu. Viumbe Wake waliohudhuria wanatushuhudia ya kwamba sisi tunawaombea watu hawa Allaah awaondoshee hiyo dhuluma, ukandamizaji na mashambulizi yaliyowapata. Tunamuomba Allaah (Jalla wa ´Alaa) aharakishe nusura yao, azihifadhi heshima zao, maisha yao, mali zao na afanye wamshinde adui wao haraka. Tunamuomba Allaah (Jalla wa ´Alaa) hilo.

Jambo la pili ni kwamba sisi tulilizungumzia hilo kitambo sana, tangu pale ambapo fitina hii ilipoanza, na tukawaambia wasifanye hivo. Ninaapa kwa Allaah ya kwamba tulisema hivo katika mnasaba wa mapinduzi ya Libya na miji mingineyo. Haya wanayajua wale waliohudhuria. Yamerekodiwa. Msifanye kitu! Mtawala hata kama atakufuru kabisa na akawa na ukafiri wa wazi haina maana kuwa tunatakiwa kumfanyia uasi papo hapo. Hili si kweli. Mtu anapaswa kutazama nguvu za watu hawa ambazo wanatakiwa kumg´oa kwa madhara madogo iwezekanavyo. Tuliwaambia wasifanye kitu na kwamba hawawezi kufanya hivo. Walijibu nini? Walisema kutwambia ya kwamba sisi ni wasaidizi wa Nusayriyyah. Sisi tunawasaidia Nusayriyyah? Ni kina nani waliokuwa wakipambana na Nusayriyyah na wakifichua upotevu wao? Je, ilikuwa ni wanachuoni na wanafunzi wa Ahl-us-Sunnah au ilikuwa hawa Hizbiyyuun? Mmoja wao alisema:

“Fanyeni uasi na msichukue si kisu wala uma!”

Yule anayetaka kukabiliana na mtawala kafiri asichukue kisu wala uma? Afanye nini? Tazama namna ambavyo hata yale maneno yao hayaingii akilini. Baadhi ya wale waliotoka kwenye TV walisema:

“Fanyeni uasi na msichukue si kisu wala uma!”

Wajihami kwa kipi? Mizinga ikawasambaratisha. Haya ndio tuliyowaambia. Lakini:

لِيَقْضِيَ اللَّـهُ أَمْرًا كَانَ مَفْعُولًا

“… ili Allaah ahukumie jambo lilokuwa lazima litendwe.” (8:44)

Tunamuomba Allaah awasamehe wale waliouawa katika waislamu hawa, awaingize Peponi na azipe familia zao subira na ujira mkubwa.

Tuliwaambia pia kuwa kama watu wanataka kukabiliana na mtu huyu, wanahitajia kuwa na nguvu ambazo watakabiliana naye kwa madhara madogo iwezekanavyo. Watu hawa hawana nguvu zozote. Watu wa syria wanahitajia nguvu.

Vikosi viwili hivi vikubwa kwa ujumla ni al-Ikhwaan al-Muslimuun na Takfiyriyyuun. Kikosi cha al-Ikhwaaniy kinasema kuwa chenyewe hakioni tatizo lolote kwa mnaswara kushika utawala au Jeshi kombozi. Ikiwa mko tayari kutawaliwa na mnaswara, kafiri wa asili, basi mnaweza vilevile kumvumilia huyo kiongozi kafiri aliyoko hivi sasa. Ni kwa nini mziweke nafsi zenu wenyewe kwenye maangamivu na kuzivunja heshima zenu? al-Ikhwaan al-Muslimuun wanasema kuwa wao hawana neno kutawaliwa na mnaswara. Haya wameyasema wao wenyewe na yamerekodiwa na ibara zao zimeandikwa magazetini. Wao hawaoni neno mnaswara kutawala. Ni kwa nini mnapigana vita sasa? Ikiwa huyu ni kafiri basi na yule mwingine pia ni kafiri, ni kwa nini basi mnataka kumg´oa kafiri na kumleta huyo kafiri mwingine?

Hapo jana msemaji wa Jeshi kombozi amesema kuwa hawana haja ya wanajeshi. Haya tuliyasema kwa miaka miwili sasa. Tuliposema hivi walisema kwamba sisi ni wasaidizi wa Nusayriyyah. Hivi sasa wale wanaowapiga vita Nusayriyyah wamesema kuwa hawawahitajii wanajeshi. Bali wamesema kwamba hawahitajii hata pesa kwa kuwa pesa zimeharibu mapinduzi. Haya nimeyasikia mwenyewe na nimeyaona kwa macho yangu na mara ya mwisho kuyasikia ilikuwa jana. Msemaji wa Jeshi kombozi amesema kuwa wanachohitajia ni silaha. Amesema kweli. Si haya ndio tulokuwa tukiyasema? Haya tuliyasema miaka miwili iliyopita. Watu wanahitajia silaha na nguvu:

تُرْهِبُونَ بِهِ عَدُوَّ اللَّـهِ وَعَدُوَّكُمْ وَآخَرِينَ مِن دُونِهِمْ لَا تَعْلَمُونَهُمُ اللَّـهُ يَعْلَمُهُمْ

“Ili muwaogopeshe kwayo maadui wa Allaah na maadui zenu na wengineo wasiokuwa wao hamwajui, lakini Allaah ndiye anawajua.” (8:60)

Wewe unachohitajia ni nguvu. Hivi sasa yeye mwenyewe anasema kuwa anahitajia silaha.

Kikosi kingine ni Takfiyriyyuun. Kwa muda si mrefu sana, takriban mwezi mmoja uliopita walikula kiapo kumpa nani? Ayman adh-Dhwaahiriy. Ni mrithi wa nani? Wa Usaamah bin Laadin. Ni kiongozi wa mtandao upi? Wa al-Qaa´idah. Ninaapa kwa Allaah lau mtaenda huko wataanza kuwaua nyinyi kabla ya kuwaua Nusayriyyah. Nawaambieni kuwa hakuna uongozi wowote wa Kishari´ah:

“Mwenye kupigana vita ili neno la Allaah liweze kuwa juu ndiye anayepigana katika njia ya Allaah.”

Hakuna. Mmesikia ule uongozi wa kijumla unaojinasibisha na Uislamu unavyosema. Mimi niko na rekodi anayetaka nimsikilize naweza kufanya hivo baada ya swalah. Wanasema kuwa wanataka serikali ya kiraia ambapo ndani yake kuna wote na wanaongoza. Hawataki utawala wa Kiislamu. Wanataka serikali ya kiraia. Hili ndilo hilo kundi linalosemwa kuwa ni la Kiislamu. Pamoja na hivyo nataka niwe mwadilifu na mwenye kuitakasa dhimma yangu na kusema kwamba wanaweza kuwepo ambao wanapigana kwa ajili ya Allaah, lakini hawana nguvu wala uongozi.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kupigana kwa ajili ya mali yake huyo ni shahidi. Mwenye kupigana kwa ajili ya heshima yake huyo ni shahidi.”

Tunataraji wale wenye kuuawa katika hali hiyo ni mashahidi. Yule mwenye kuwajia na kutaka kuwapokonya hayo, tunawaambia ndugu zetu wapambane na wazitetee nafsi zao. Ama nyinyi kuwawajibishia watu wote waje huko ilihali wao wenyewe wanasema kuwa hawana haja ya wanajeshi? Ni nini alichofanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa fai ambayo Allaah amempa achukue sehemu yake? Alikuwa akiwapa jamaa zake na akiwapa matumizi familia yake kwa mwaka mmoja. Pesa zinazobaki anaziweka katik ngao na silaha. Alikuwa akinunua farasi, ngamia, silaha, mikuki na ngao. Watu hawa wanayahitajia haya. Wangelikuwa na silaha mgeliona namna hali inavyobadilika. Hivi sasa wana silaha chache ilihali maadui wao wana silaha nyingi na wanawashinda kwa silaha za ndege. Hii ndio hali yao.

Sisi pindi tunaposema kuwa hakuna Jihaad ya Kishari´ah tunaelewa nini maana ya maneno haya hata kama al-Ikhwaan al-Muslimuun watakasirika. Sisi tunawaambia njooni na mtueleze ni kwa nini wanapigana. Ili neno la Allaah liweze kuwa juu? Wamekwishasema wazi ya kwamba hawana neno kutawaliwa na mtu kafiri. Ni nchi gani hii ya Kiislamu mnayoita? Himdi zote ni za Allaah ambaye amewafichua kwa maneno yao wenyewe. Hata hivyo misaada ya Allaah kwa Ahl-us-Sunnah, Salafiyyuun, inaonekana mibaya. Hawana sura yoyote kwenye vyombo vya khabari. Vinginevyo lau ingeliwekwa wazi hadharani basi wangeliangamia al-Ikhwaan al-Muslimuun wote. Nazungumzia kuhusu kundi hili ambalo limepelekea shari katika miji yote ya Kiislamu. Wanalingania katika kuwakufurisha watawala na wanasema kuwa watawala wana kirafiki na magharibi, makafiri, mayahudi na manaswara. Uhalisia wa mambo watu wa kwanza walioandika nao mkataba na wakawafanya mayahudi na manaswara marafiki ni wao wenyewe! Ni ajabu iliyoje! Lakini akili za watu zimeenda wapi? Sijui. Baadhi ya watu unahitajia kuwaleta kwenye mwanga na kuwaeleza kuwa unaangaza. Hawaoni. Kwa hivyo watu wanahitajia kuwa na subira. Subira – Allaah akitaka – inapelekea katika matunda. Watu wanahitajia kupewa ujuzi na elimu. Wawaulize watu wa Misri ni kipi kinachoendelea kwao. Matatizo makubwa katika ulinganizi wa dini ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Walinganizi wa kweli, sio watu wa mapinduzi, na waongozaji wenye kuwaongoza watu katika dini ya Allaah wamefunikwa. Ni wenye huruma zaidi kwa watu kuliko nafsi zao wenyewe. Watu wanajitupa wao wenyewe kwenye maangamivu ilihali hawa wanawazuia. Mnajua ni kwa nini wanafanya hivo? Kwa wao ni warithi wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mfano wangu mimi na nyinyi ni kama mfano wa mtu aliyekonga moto. Wanyama na vipepeo hawa wakaanza kuingia ndani yake na kumshinda. Nashika ncha za izaar zenu ilihali nyinyi mnanishinda na kuingia ndani yake. Huo ndio mfano wangu mimi na nyinyi. Mimi nimezishika ncha za izaar zenu ili msiingie ndani ya moto: “Tahadharini na moto! Tahadharini na moto!” Lakini nyinyi mnanishinda na kuingia ndani yake.”

Wanachuoni ndio warithi wa Mitume. Moto huu ni mwanga lakini anayeunguza. Asiyejua namna ya kuutumia anaunguzwa nao. Namna hii ndivyo zinavyokuja fitina. Zinaangaza. Wanachuoni wanachukua nafasi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wanazishika ncha za izaar za watu na kuwazuia na moto. Lau watawaacha wanakuwa kama vipepeo hawa vinavyodhani kuwa mwangaza huu ni nuru na matokeo yake wanaingiza ndani yake na kuteketea. Wanachuoni wako na mwanga. Wanakuzuia kuingia ndani ya moto. Ama kuhusu watu hawa, wanakuonyesha sura ya moto kuwa mwanga. Unapoanza kuukaribia, unatumbukia ndani ya moto kwa nguvu na kwa kutokutaka. Hii ndio tofauti ya wanachuoni wa Ahl-us-Sunnah walio na uelewa na elimu katika dini na watu wanaopelekwa na hisia na huruma au ni katika watu wanaofuata matamanio.

  • Mhusika: Shaykh Muhammad bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.youtube.com/watch?v=8v1nA4fHoTE
  • Imechapishwa: 08/04/2017