Sababu ya kujitokeza kwa wanafiki

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّـهِ وَبِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَمَا هُم بِمُؤْمِنِينَ

“Miongoni mwa watu wako wasemao “Tumemuamini Allaah na Siku ya Mwisho hali ya kuwa si wenye kuamini.”[1]

Tambua kwamba unafiki ni kule kuonyesha kheri na kuficha shari. Katika maana hii kunaingia unafiki wa kiimani na unafiki wa kimatendo. Unafiki wa kimatendo ni ule uliyotajwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

“Alama za mnafiki ni tatu; anapozungumza husema uongo, anapoahidi anakwenda kinyume na anapoaminiwa hufanya khiyana.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Anapogombana basi hufanya uovu.”

Kuhusu unafiki wa kiimani ambao unamfanya mtu kutoka nje ya Uislamu ndio ule ambao Allaah amewaeleza wanafiki katika Suurah hii na nyenginezo.

Unafiki haukuweko kabla ya kuhajiri kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutoka Makkah kwenda Madiynah. Baada ya kuhama na kukatokea vita vya Badr ambapo Allaah alawadhihirisha waumini na kuwatukuza ndipo wakadhalilika wale walioko Madiynah ambao bado hawajaingia katika Uislamu. Kipindi hicho ndipo baadhi yao wakadhihirisha Uislamu kwa ajili ya khofu na hadaa. Lengo lingine ilikuwa kuisalimisha damu na mali yao. Wakawa kati ya waislamu kwa nje wakionekana kuwa pamoja nao ilihali ukweli wa mambo hawako pamoja nao. Kutokana na upole wa Allaah kwa waumini ndipo akawaanika na kuwasifu kwa sifa ambazo zitawapambanua ili waumini wasije kudanganyika nao na kusalimika na mengi katika maovu yao.

[1] 02:08

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-Kariym, sid. 31
  • Imechapishwa: 06/05/2020