Sababu ya Ibn-ul-Jawziy kutunga kitabu “Ahkaam-un-Nisaa´”

Mimi daima ni mwenye kuhimiza elimu, kwa sababu elimu ndio nuru ambayo mtu anaongozwa kwayo. Hata hivyo nimeona kuwa wanawake ndio wenye haja zaidi ya kuzindushwa kutoka katika ndoto hii yenye kushtua kuliko wanamme. Kwani wao wako mbali zaidi na elimu na wanaacha matamanio yawapeleke.

Mara nyingi msichana anakulia pasi na kufunzwa Qur-aan. Hajui namna ya kujitwahirisha kutokamana na hedhi na wala hajifunzi nguzo za Uislamu. Hafunzwi haki za mume isipokuwa wakati wa kuolewa. Pengine akamuona mama yake anachelewesha kujisafisha na hedhi mpaka pale anapofua nguo zake na akaingia bafuni bila ya kujisitiri na huku akisema:

“Siko na mwengine zaidi ya mama na dada yangu.”

Akachukua mali kutoka kwa mume wake bila ya idhini yake.

Akamroga na kudai kuwa inafaa kufanya hivo kwa ajili avutikiwe naye.

Akaswali kwa kuketi pamoja na kwamba anao uwezo wa kusimama.

Anafanya majaribio ya kuiharibu mimba pindi anaposhika ujauzito. Tutataja magonjwa mengi huko mbele ya kitabu yanayofahamisha ughafilikaji huu uliotajwa.

Akifaulu na akahudhuria vikao vya wapiga visa, basi hilo huwa baya na lenye madhara zaidi kwake. Baadaye atakuja kuonyesha mapambo yake na watu waje kufitinika naye na yeye mwenyewe aje kufitinishwa nao. Vilevile atakuja kufitinishwa na wapiga visa. Wanatia sumu badala ya kuponya. Husoma mashairi ya mapenzi ya haramu na nyimbo. Pindi mambo hayo yanapokutana na moyo mtupu, basi inakuwa vigumu kuyaondosha.

Hawatilii umuhimu kufunza mambo ya wajibu na kukataza mambo yaliyokatazwa. Pengine akawaona wanamme waliopo wanapiga makelele na hivyo na yeye akapiga makelele.

Nilipoona kuwa wanawake wana haja kubwa zaidi ya elimu kuliko wanamme, ndipo nikaanza kutunga kitabu hiki ambacho kinazungumzia hali zao. Nimefanya hivo hali ya kutarajia ujira. Sijamuona mwengine aliyenitangulia kuandika kitabu mfano wake.

Wanawake hata kama ni wenye kupuuziliwa mbali na suala la elimu, wanapatikana siku zote wanawake wazuri wenye kutafuta elimu. Inawezekana wakazungumzishwa lukuki ya watu lakini mwenye kuitikia akawa mtu mmoja. Muusa (´alayhis-Salaam) alimuonya Fir´awn na watu wake ambao walikuwa maelfu ya watu, lakini hakuna aliyeitikia isipokuwa Harsal na Aasiyah.

  • Mhusika: Imaam ´Abdur-Rahmaan bin al-Jawziy al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-un-Nisaa’, uk. 9-10
  • Imechapishwa: 21/04/2020