Sababu ya Ahl-us-Sunnah kuyaingiza mambo haya katika `Aqiydah

Hichi ni kitabu kinachoitwa “Lum´at-ul-I´tiqaad” ni katika vitabu vifupi kuhusu ´Aqiydah. Kimezungunzia masuala ya ´Aqiydah na wanachuoni baada ya mtunzi wa kitabu wamekisifu sana.

Mambo ya ´Aqiydah kwa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah yamejengwa juu ya kufafanua misingi sita ya imani, nayo ni kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake, siku ya Mwisho na Qadar – kheri na shari yake – ni yenye kutoka kwa Allaah (Ta´ala). Kumuamini Allaah kumejumuisha ndani yake kuamini kuwa Allaah ni Mmoja katika uungu Wake na Yeye ndiye mwenye kustahiki kuabudiwa pasi na mwengine, kuamini majina na sifa Zake (Jalla wa ´Alaa) na kwamba Yeye amepwekeka katika hayo, hakuna anayeshabihiana na kufanana Naye. Mwanzoni mwa Uislamu, katika zile karne za kwanza, hakukuwepo haja ya kuitenga Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah kivyake kwa njia ya upambanuzi pindi kulipokuwa kunazungumziwa mada hii, yaani kumuamini Allaah. Badala yake mtu alikuwa anatosheka kufafanua imani hii kwa jumla ili waislamu wasije wakatumbukia katika shirki na ilili shirki isije kudhihiri. Kwa hivyo vitabu vingi vya ´Aqiydah vyenye kuzungumzia juu ya kumuamini Allaah karibu vyote vilikuwa vinahusu majina na sifa za Allaah. Kwa ajili hiyo ndio maana hutopata katika kitabu hichi kumezungumziwa kwa upambanuzi juu ya Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Hili walilifanyia kazi wanachuoni waliokuja baada ya kufa kwa mtunzi wa kitabu. Hata hivyo utapata kumezungumziwa kwa upambanuzi juu ya majina na sifa za Allaah. Hili ni kutokana na haja ya hilo katika zama za mtunzi wa kitabu hichi. Kadri na jinsi waja wana haja ya kufafanuliwa zaidi jambo fulani, ndivyo jinsi wanachuoni walivyolitendea kazi kwa bidii. Kwa ajili hiyo wakaandika vitabu kuhusu Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah, kwa mfano Kitaab-ut-Tawhiyd, Kash-ush-Shubuhaat, Thalaathat-ul-Usuwl na mfano wake. Kwa sababu ya kukidhi haja ya kipindi hicho vitabu hivi vikafafanua Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah, msingi wa nguzo ya kwanza ya kuamini, ambayo ni kumuamini Allaah.

Baada ya hapo mwandishi akataja kuwaamini Malaika, Vitabu Vyake, Mitume Wake, siku ya Mwisho na Qadar kheri na shari yake.

Baada ya kufafanuliwa nguzo sita za imani, mwandishi akataja mambo zaidi kuhusu I´tiqaad. Mambo hayo hayana lolote kuhusiana na I´tiqaad, lakini yameingizwa katika mambo ya ´Aqiydah kwa sababu Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wameenda kinyume na Ahl-ul-Bid´ah wal-Furqah katika mambo hayo. Mfano wa mambo hayo ni kama kuwazungumzia Maswahabah, mama wa Waumini na haki zao. Mwandishi ametaja pia kuhusu uongozi katika Uislamu na yale mambo yenye kuwawajibikia watawala na wananchi; mambo ambayo Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wametofautiana kwayo na Khawaarij, Mu´tazilah na watu mfano wao.

Vilevile Ahl-us-Sunnah wameingiza kupangusa juu ya soksi katika mambo ya ´Aqiydah. Hili ni kwa sababu ya kwenda kinyume na wale wenye kuonelea kuwa kupangusa juu ya soksi si sahihi. Kadhalika wametaja karama za mawalii na yale Allaah anayoyapitisha kupitia mikono yao katika mambo mbalimbali ya elimu, ya ajabu, ya uwezo na yenye kuathiri. Haya yametajwa kwa upambanuzi na kufafanuliwa kwa sababu kuna ambao wanaenda kinyume na karama hizi, ima kwa kuzikanusha, kama wanavyofanya Mu´tazilah, au kupetuka mipaka kwa mawalii kiasi cha kwamba kuna waliowafanya nafasi za mawalii zikawa juu ya za Mitume.

Kadhalika mambo ya maadili yanatajwa katika mambo ya ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

Kwa hivyo ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah imekusanya mambo yote haya na haihusiani peke yake na kuamini majina na sifa za Allaah, siku ya Mwisho na Qadar kheri na shari yake. Bali ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah imekusanya mambo yote haya, kwa sababu wao katika mambo haya wametofautiana na Ahl-ul-Bid´ah waz-Zaygh ambao wanayarudisha Maandiko, na wala hawafuati Sunnah na hawaachi wakahukumiwa kwavyo kuhukumiwa kikamilifu. Kwa njia hiyo Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wakawa ni wenye sifa za kipekee kwa sababu wanaiadhimisha Sunnah na watu wake na wanawakosoa wale wenye kwenda nayo na kwenda kinyume na maimamu wao.

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Lum´at-il-I´tiqaad (01)
  • Imechapishwa: 06/09/2020