Ramadhaan inasamehe madhambi yote ya mtu?


Swali: Shaykh umetaja mwanzoni mwa mkutano ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kufunga Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”

Je, inahusu vilevile madhambi makubwa na madogo na haki za watu? Naomba upambanuzi Allaah akuwafikishe.

Jibu: Hadiyth hii imekuja kwa jumla:

“… atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”

Inajumuisha na kupelekea ya kwamba madhambi yote ni yenye kusamehewa. Lakini ujumla huu unafanywa maalum kwa dalili zengine zinazofahamisha ya kuwa ni lazima kujiepusha na madhambi makubwa. Dalili ya hilo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah tano, swalah ya ijumaa mpaka swalah ya ijumaa nyingine na Ramadhaan mpaka Ramadhaan nyingine ni vyenye kufuta yaliyo kati yake midhali kutaepukwa madhambi makubwa.”

Ramadhaan mpaka Ramadhaan nyingine hapa kunamaanishwa kuifunga na kusimama nyusiku zake.

Kujengea juu ya haya ujumla huu unakuwa ni wenye kufanywa maalum kwa Sunnah kwa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hivyo usitamani ambavyo si haki kwako na usikate tamaa kwa ambayo ni haki kwako. Wewe unachotakiwa ni kufunga na usimame Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio na nakubashiria kheri.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (33) http://binothaimeen.net/content/739
  • Imechapishwa: 13/05/2018