Radd kwa Khawaarij na Mu´tazilah wanaopinga uombezi


Kuhusu utata wa wale wenye kupinga kuwepo kwa uombezi. Wenye kupinga ni Mu´tazilah na Khawaarij. Wamekanusha uombezi na wamekanusha vilevile kutoka kwa yeyote ndani ya Moto ikiwa ataingia. Wametumia dalili kwa maneno ya Allaah (Ta´aa).

Dalili ya kwanzaAllaah (Ta´ala) anasema:

وَاتَّقُوا يَوْمًا لَّا تَجْزِي نَفْسٌ عَن نَّفْسٍ شَيْئًا وَلَا يُقْبَلُ مِنْهَا شَفَاعَةٌ وَلَا يُؤْخَذُ مِنْهَا عَدْلٌ

“Iogopeni Siku ambayo nafsi haitaifaa nafsi nyingine kwa kitu chochote kile na wala haitakubaliwa kutoka kwake uombezi na wala hakitachukuliwa kutoka kwake kikomboleo.” (02:48)

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنفِقُوا مِمَّا رَزَقْنَاكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ يَوْمٌ لَّا بَيْعٌ فِيهِ وَلَا خُلَّةٌ وَلَا شَفَاعَةٌ

“Enyi mlioamini! Toeni katika Tulivyokuruzukuni kabla haijafika siku ambayo hakutakuweko mapatanohumo wala urafiki wala uombezi.” (02:254)

Wamesema kuwa Aayah hizi zinatoa dalili kuonesha kuwa mwenye kuingia Motoni miongoni mwa waislamu wenye madhambi makubwa watadumishwa humo na uombezi juu yao hautokubaliwa.

Jibu: Aayah hizi zinawahusu makafiri peke yao. Kinachotilia nguvu hilo ni mazingira ya mazungumzo katika Aayah ya tatu. Aayah imeteremka ikiwaraddi mayahudi kwa kudai kwao kuwa mababu zao watawashufaia.

Dalili ya pili: Wametumia dalili kwa maneno ya Allaah (Ta´ala):

فَمَا تَنفَعُهُمْ شَفَاعَةُ الشَّافِعِينَ

“Basi hautowafaa uombezi wowote wa waombezi.” (74:48)

Wanacholenga ni kutaka kusema kuwa imeonyesha kuwa muislamu mwenye dhambi kubwa uombezi hautomfaa kitu.

Jibu: Aayah inawahusu makafiri. Hilo ni kutokana na dalili ya kuelezwa kwao katika Aayah ilio kabla yake ambapo amesema (Ta´ala):

مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَرَ

[Watawauliza]: “Nini kilichokuingizeni katika [Moto wa] Saqar?” (74:42)

mpaka aliposema:

وَكُنَّا نُكَذِّبُ بِيَوْمِ الدِّينِ

“Na tulikuwa tunaikadhibisha siku ya Malipo.” (74:46)

Dalili ya tatu: Wametumia dalili kwa maneno ya Allaah (Ta´ala):

مَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ حَمِيمٍ وَلَا شَفِيعٍ يُطَاعُ

“Madhalimu hawatokuwa na rafiki wa dhati na wala mwombezi anayetiiwa.” (40:18)

Wanacholenga ni kutaka kusema kuwa Aayah imeonyesha kuwa dhalimu hatokuwa na rafiki mwenye kutiiwa. Mtenda maasi ni dhalimu.

Jibu: Makusudio ya neno “madhalimu” ni makafiri. Kwa sababu kunaposemwa neno “dhuluma”, linaenda katika kufuru. Kwa kuwa kufuru ndio dhuluma ilio kubwa. Dalili ya hilo ni maneno ya Allaah (Ta´ala):

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

“Usimshirikishe Allaah, hakika shirki ni dhuluma kubwa.” (31:13)

Dalili ya nne: Wametumia dalili kwa maneno ya Allaah (Ta´ala):

رَبَّنَا إِنَّكَ مَن تُدْخِلِ النَّارَ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ

“Mola wetu! Hakika Umuingizaye Motoni kwa yakini Umemfedhehesha.” (03:192)

Wanacholenga ni kutaka kusema kuwa Aayah imeonyesha kuwa yule mwenye kuingia Motoni basi huyo ni mwangamivu na uombezi hautomfaa kitu. Badala yake mtu kama huyo ni mwenye kutengwa mbali, mwenye kuchukiwa na si mwenye kuridhiwa. Hivyo haingii katika maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

“Na wala hawamuombei yeyote isipokuwa kwa yule ambaye Amemridhia.” (21:28)

Kwa kuwa yule ambaye amefedheheshwa na Allaah hawezi kumridhia.

Jibu: Makusudio ya:

تُدْخِلِ النَّارَ

“Umuingizaye Motoni.” (03:192)

bi maana umdumishaye. Yule mwenye kudumishwa Motoni ni mwangamivu na uombezi ni kweli hautomnufaisha kitu. Kwa kuwa kudumishwa Motoni itakuwa ni jambo maalum kwa yule aliyekufa katika kufuru.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/329-330)
  • Imechapishwa: 21/05/2020