Kuhusu wale wenye kupinga kuwa Allaah ataonekana Aakhirah kama mfano wa Jahmiyyah, Mu´tazilah na waliowafuata katika Ibaadhiyyah Khawaarij na Imaamiyyah wana utata wa kiakili na wa Kishari´ah. Makusudio ya utata ni dalili, lakini hata hivyo pale ambapo mtoaji dalili anapokuwa hakupatia dalili zake huitwa kuwa ni utata.

Kilichowapelekea kufanya hivi ni kwa sababu ya kuitegemea kwao akili. Mu´tazilah wenye kupinga kuonekana Allaah Aakhirah akili kwao ndio msingi. Balaa lao ndio limewafanya kutanguliza kwao akili juu ya andiko na kuifanya akili ndio msingi na kuweka Kitabu cha Allaah nyuma ya migongo yao. Walipotegemea akili ndio wakawa wamefasiri maandiko kimakosa yenye kuthibitisha kuwa Allaah ataonekana Aakhirah. Pale ambapo wakanushaji akili ndio waliifanya kuwa msingi wao wakawa wameyapotosha maandiko kutoka katika Qur-aan na Sunnah ili yaweze kuafikiana na akili zao. Miongoni mwa utata wa kiakili wa wale wenye kupinga kuonekana kwa Allaah Aakhirah ni pamoja na:

Mosi: Wamesema ili kuthibitisha kuonekana kwa Allaah basi ni lazima Allaah awepo upande fulani. Akishakuwa upande fulani basi ni lazima awe na mwili na awe na kikomo na ilihali Allaah hayuko upande fulani na hana kikomo. Hivyo tukithibitisha upande ina maana ni kumtukana Allaah. Wanasema “Allaah hayuko upande fulani na kila kisichokuwa upande fulani hakitoonekana” na hivyo natija inakuwa “Allaah hatoonekana.” Hii ni dalili ya kimantiki ambayo imejigawa na vitangulizi viwili; “Allaah hayuko upande fulani”, kitangulizi cha kwanza; “kila kisichokuwa upande fulani hakionekani”, kitangulizi cha pili. Hatimae kitangulizi cha kwanza na cha pili kinatoa natija ifuatayo: Hivyo Allaah hatoonekana. Wewe ukijisalimisha kwao kwa kuwakubalia vitangulizi hivyo viwivili basi wanakulazimisha natija.

Wewe la kufanya hapa ni kwamba pingana na kitangulizi cha kwanza na usiwakubalie nacho au pingana na kitangulizi cha pili na usiwakubalie nacho. Au pinga kabisa vitangulizi vyote viwili hivi ili natija ibatilike. Majibu ya utata huu ni haya yafuatayo:

1 – Mnakusudia nini kwa neno “upande”. Mnasema kuwa ili kuthibitisha kuwa Allaah ataonekana basi ni lazima awepo upande fulani, ni yapi makusudio yenu kwa neno “upande”; kwa neno lenu “upande” mnakusudia kitu kilichopo au kitu kisichopo? Kwa neno lenu “upande” mnakusudia kitu kilichoumbwa au kitu kisichopo? Ni jambo lenye kujulikana ya kwamba katika ulimwengu huu hakuna isipokuwa Muumba na viumbe tu. Ikiwa kwa neno lenu “upande” mnakusudia kitu kilichopo bi maana kilichoumbwa, basi Allaah ametakasika kuwa sehemu iliyoumbwa. Allaah hayuko katika kitu kilichoumbwa. Allaah hakuingia katika kitu kilichoumbwa na wala katika viumbe Vyake hakuna chochote katika Dhati Yake. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ametengana na viumbe Vyake. Ikiwa kwa neno lenu “upande” mnakusudia upande uliyoumbwa ndio yuko ndani yake na kukomeka humo na kumzunguka, basi Allaah ametakasika na upande kwa maana kama hii. Kwa sababu Allaah hayuko katika upande kutoka katika viumbe Vyake na hayuko katika kitu katika viumbe Vyake na hawi ndani ya kitu katika viumbe Vyake na hakomeki kwenye kitu katika Viumbe Vyake (Subhaanahu wa Ta´ala). Hakika Yeye ni Mkubwa, Yuko juu na ametukuka na hilo. Allaah ametengana na viumbe Vyake (Subhaanahu wa Ta´ala). Allaah hayuko katika upande kwa maana hii.

Ikiwa kwa neno lenu “upande” mnakusudia kitu kisichokuwepo ambacho hakikuumbwa, nacho ni kile kilichoko juu ya ´Arshi, basi kupinga kwenu upande kwa maana hii ni batili. Allaah yuko katika upande wa juu baada ya kuisha kwa viumbe ambapo mwisho wake ni paa ya ar-Rahmaan. Hivyo ni lazima kufafanua.

Kwa neno lenu “upande” ikiwa mnakusudia kitu kilichoumbwa, basi Allaah hayuko katika upande. Na kwa neno lenu “upande” ikiwa mnakusudia kitu kisichokuwepo nacho ni kile kilichoko juu ya ´Arshi, basi Allaah yuko katika upande kwa ibara hii. Kujengea juu ya haya, tunasema:

Kitangulizi chenu cha kwanza ni batili. Kule kusema kwenu kuwa Allaah hayuko upande fulani, ikiwa mnakusudia kitu kisichokuwepo basi tunasema kuwa kitangulizi chenu hichi ni batili na wala hakuna dalili ya kuthibiti kwake. Badala yake tunasema kuwa Allaah yuko upande fulani ikiwa ni kwa maana hii. Kwa sababu upande ni kitu kisichokuwepo na hivyo ina maana ya kwamba Allaah yuko kwa juu, juu ya ´Arshi. Kwa neno lenu “upande” ikiwa mnakusudia kitu kilichopo, basi kitangulizi chenu cha pili kimebatilika. Nacho ni kile kinachosema kuwa kila kisichokuwepo upande fulani hakionekani. Kwa sababu kila chenye kuonekana sio lazima kiwe katika upande uliyoumbwa. Eneo la juu la ardhi linaweza kuonekana pamoja na kwamba ulimwengu hauko katika ulimwengu mwingine. Hailazimishi kuwepo mlolongo ambapo ulimwengu uwepo katika ulimwengu mwingine na ulimwengu mwingine katika ulimwengu mwingine na kuendelea mbele pasina kuweka kikomo. Vitangulizi vyote viwili vikibatilika au kimoja wapo, basi natija pia – ambayo inasema kuwa Allaah hatoonekana – inakuwa ni yenye kubatilika. Hii ni dalili ya kwanza ya kiakili.

Pili: Dalili ya pili ya wale wenye kupinga kuonekana kwa Allaah (´Azza wa Jall) wamesema kuwa Allaah hana mwili, hayuko ndani ya ulimwengu wala nje yake, kilicho na wasifu kama huo hakiwezi kuonekana. Dalili hii ya kiakili inajibiwa kwa majibu mawili yafuatayo:

1 – Jibu la kwanza: Kuthibitisha kitu kisichopo ndani ya ulimwengu wala nje yake ni jambo ambalo haliwezi kuhisiwa. Hukumu ya kimaumbile inapelekea kuthibitisha kitu au jambo ambalo haiwezekani likahisiwa.

2 – Jibu la pili: Tumejisalimisha kuwepo kwa jambo au kitu ambacho hakiwezi kuhisiwa, kuwepo kwa kitu ambacho kinaweza kuhisiwa ni aula zaidi. Hivyo basi, yule mwenye kuthibitisha kilichopo juu ya ulimwengu kisichokuwa na mwili na ambacho anaweza kukihisi, basi maneno yake yako karibu zaidi ya uingiaji akilini kuliko mwenye kuthibitisha kilichopo ambacho hawezi kukihisi na wakati huo huo kikawa hakiko ndani ya ulimwengu wala nje yake.

3 – Jibu la tatu: Kuona kitu kisichokuwa na mwili wala kuwepo upande fulani, ima iwe ni kitu ambacho akili inakipitisha [kuingia akilini na kukisapoti] au iwe ni kitu ambacho inakipinga. Ikikipitisha, hakuna namna kabisa ya kufanya hivo. Na ikiwa akili haitokubaliana na jambo hilo, basi kule akili kupingana na kuwepo kwa kitu kisichopo ndani ya ulimwengu wala nje ya ulimwengu, kupinga huko kuna nguvu zaidi na zaidi.

4 – Jibu la nne: Kumuona Allaah (Ta´ala) ima iwe ni jambo ambalo linawezekana au iwe ni jambo lisilowezekana. Ikiwa ni jambo linalowezekana, basi maneno yenu ya kuthibitisha kuwepo kwa kitu ambacho hakiwezi kuhisiwa yatakuwa yamebatilika ambayo yanasema kisichokuwepo ndani ya ulimwengu wala nje ya ulimwengu. Na ikiwa mtasema kuwa kumuona ni jambo lisilowezekana, basi hapo mtaambiwa kuwa hawezi kuhisiwa na hivyo haitokubaliwa hukumu ya kubahatisha.

Hapo itakuwa imethibiti kuwa kumuona Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ni jambo lenye kulingana na Yeye na sio kama jinsi ya kuonekana vitu vya kawaida vilivyo na miili.

Hizi ni dalili za kiakili ambazo wapinzani wamezishikilia. Dalili kwa dalili. Dalili za kiakili zinaraddiwa vilevile na dalili za kiakili.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/234-237)
  • Imechapishwa: 27/05/2020