Ahl-ul-Bid´ah wameyajibu maandiko haya kutoka katika Qur-aan na Sunnah kwa kuyapindisha [Ta´wiyl] na kuyapotosha [Tahriyf]. Wamesema kupitia ndimi ya Bishr al-Mirriysiy ambaye alikuwa ni Jahmiy Mu´taziliy ya kwamba makusudio ya kuonekana kwa Allaah Aakhirah katika Hadiyth hizi ni kumuona kwa moyo ambako ni ujuzi. Maana ya maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mtamuona Mola Wenu kama mnavouona mwezi”

makusudio yake ni kwamba mtamjua Mola Wenu pasina wasiwasi wowote wala mashaka kama jinsi mnavojua mwezi kuwa huu ndio mwezi na kuwa makusudio sio kumuona kwa macho. Wanasema kuwa nyinyi Mushabbihah – wakikusudia kwa kusema hivo Ahl-us-Sunnah – mmefikiria kuwa makusudio ni kumuona kwa macho jambo ambalo ni kufananiza kwenu na ni kumtukana Mola. Wanasema kuwa makusudio sio kumuona kwa macho kwa kuwa huku ni kushabihisha na kumfanya Allaah kuwa na mwili. Wanasema kuwa makusudio ni kumuona kwa moyo. Wamesema kuwa lugha ya kiarabu ni yenye kutolea dalili kwa wanayoyasema. Waarabu humwambia kipofu:

“Kipi kimechomfanya kuona”

wakiwa na maana ya:

“Kipi kimemfanya kujua”

Makusudio ni ujuzi.

Waarabu husema pia:

“Nimeyatazama mambo”

wakiwa na maana ya kuyajua mambo. Hawakusudii kuona kwa macho kama mnavofikiria kwa sababu Allaah amejikanushia hilo pale aliposema:

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ

“Macho hayamzunguki bali Yeye anayazunguka macho yote – Naye ni Mpole, Mjuzi wa yote.” (06:103)

Wakaendelea kusema kuwa kuna dalili ya maandiko mengi juu ya yale wanayoyasema kwamba kuonekana inakuwa kwa maana ya ujuzi ikiwa ni pamoja na Kauli Yake (Ta´ala):

أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِأَصْحَابِ الْفِيلِ

“Je, huoni jinsi Mola wako Alivyowafanya watu wa ndovu?” (105:01)

bi maana hamjui. Ni dalili yenye kuonesha kuwa neno “kuonekana” lililokuja katika maandiko haya makusudio yake ni ujuzi. Haya ndio majibu ya wale wenye kupinga kuonekana kwa Allaah kwa maandiko tuliyoyatoa. Ahl-us-Sunnah wamejibu vipingamizi hivi kwa majibu mengi ikiwa ni pamoja na:

Jibu la kwanza: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefasiri neno “kuonekana” katika Hadiyth hizi ya kwamba ni kuonekana kwa macho. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameiwekea nguvu tafsiri hii kwa Hadiyth. Anayetaka kupindisha maana atafedheheka. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mtamuona Mola Wenu kama mnavouona mwezi.”

Hapa ni jambo la wazi wazi lenye kuonesha kuwa makusudio ni kuona kwa macho.

Jibu la pili: Kufasiri neno “kuoenekana” kuwa ni kumtambua ni tafsiri yenye kwenda kinyume na tafsiri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pamoja na ukiongezea juu ya hilo ni kwamba haikupokelewa kutoka kwa mwanachuoni yeyote aliyesema kuwa makusudio ya “kuonekana” katika Hadiyth hizi ni elimu. Isipokuwa labda msomi ambaye ni mjinga na mpotevu. Vipi basi mtaacha tafsiri ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambayo inatiliwa nguvu na Hadiyth na kufuata tafsiri ya msomi ambaye ni mjinga na tena isitoshe mpotevu asiyekuwa na mashiko yoyote na hakupokea kutoka kwa mwanachuoni yoyote?

Jibu la tatu: Wasomi wa lugha wameafikiana juu ya kwamba kukutana kunakuwa ana kwa ana kwa macho. Abul-´Abbaas Ahmad bin Yahyaa ambaye anajulikana kwa jina la “Tha´lab” amenukuu maafikiano ya wanawasomi wa lugha ya kiarabu kwamba makusudio ya kukutana katika Kauli ya Allaah (´Azza wa Jall):

وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيمًا تَحِيَّتُهُمْ يَوْمَ يَلْقَوْنَهُ سَلَامٌ ۚ وَأَعَدَّ لَهُمْ أَجْرًا كَرِيمًا

“Naye daima kwa waumini ni mwenye kuwarehemu. Maamkizi yao Siku watakayokutana Naye “as-Salaam” [amani] na Amewaandalia ujira mtukufu.” (33:43-44)

ya kwamba makusudio ya neno “kukutana” ni kuona kwa macho. Amenukuu kutoka kwao kwa mlolongo wa wapokezi ambao ni sahihi. Wasomi wa lugha ya kiarabu wamekubaliana juu ya kwamba kukutana inakuwa ana kwa ana kwa kuona kwa macho.

Dalili ya nne: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtamuona Mola Wenu kama mnavouona mwezi.”

hii inakuwa na maana kama ifuatayo:

Mtamuona Mola Wenu kama jinsi unavyoonekana mwezi na jua. Ni jambo lenye kujulikana kuwa sisi tunaona jua na mwezi kwa macho yetu kwa upande wa juu. Kuonekana kwa Allaah ni lazima kuwe vivyo hivyo kwa macho hali ya kuwa juu.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/225-227)
  • Imechapishwa: 23/05/2020