Swali: Moja katika utata wa manaswara ni kuwa wanasema kwamba ´Iysaa ni bora kuliko Muhammad kwa kuwa ´Iysaa hana baba na Muhammad yeye yuko na baba. Hivyo wanamnasibisha ´Iysaa kwamba ni mwana wa Allaah. Vipi tutaraddi hilo?

Jibu: Allaah hana mwana wala mtoto. Wanamkufuru Allaah na hawakumtakasa Allaah kutokana na mapungufu, mtoto na wake. Ni nani mwenye kumtakasa Allaah kutokana na mapungufu na kuamini kuwa hakuzaa na wala hakuzaliwa na wala hakuna yeyote anayelingana Naye au ni yule mwenye kuamini imani ya utatu, kwamba ´Iysaa bin Maryam ndiye Allaah na kwamba ´Iysaa ni mwana wa Allaah? Hawa wamemtakasa Allaah? Ni waongo.

Muhammad ndio Mtume na Nabii bora. Fadhila zinatokamana na Allaah; anampa yule Anayemtaka. Hakuna awezae kumzuia Allaah kumfadhilisha mja Amtakaye pasi na wengine. Allaah ndiye mjuzi zaidi ni wapi pa kuziweka fadhila na neema Zake na ni nani anayezistahiki. Allaah (Subhanaahu wa Ta´ala) ndiye mjuzi zaidi. Sisi hatupingani na Allaah (´Azza wa Jall). ´Iysaa sio mwana wa Allaah, kama wanavyosema. Allaah alimuumba ´Iysaa kwa neno “Kuwa!”:

خَلَقَهُ مِن تُرَابٍ ثُمَّ قَالَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

“Amemuumba kutokana na udongo kisha Akamwambia: ‘Kuwa!` basi akawa.” (03:59)

Kwa neno hili ndio akawa ´Iysaa (´alayhis-Salaam), bila ya baba. Ndio maana anaitwa kuwa ni “neno la Allaah”, kwa sababu Allaah alimuumba kwa neno pasi na baba. Hakika ana fadhila kwa vile Allaah alimuumba kwa neno bila ya baba. Hata hivyo sio mwana wa Allaah. Allaah hana mwana:

لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ

“Hakuzaa na wala Hakuzaliwa.” (112:03)

Ikiwa hii ni fadhila ya ´Iysaa kwa vile aliumbwa bila ya baba, basi Aadam ana haki zaidi ya fadhila, kwa sababu Allaah alimuumba bila ya mama wala baba:

إِنَّ مَثَلَ عِيسَىٰ عِندَ اللَّـهِ كَمَثَلِ آدَمَ ۖ خَلَقَهُ مِن تُرَابٍ ثُمَّ قَالَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

“Hakika mfano wa ‘Iysaa kwa Allaah ni kama mfano wa Aadam. Amemuumba kutokana na udongo kisha Akamwambia: ‘Kuwa` basi akawa.” (03:59)

Alisema kumwambia ´Iysaa “Kuwa!” na akawa. Ikiwa hii ni hoja basi Aadam ni bora kuliko ´Iysaa.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Tafsiyr-ish-Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (15) http://www.alfawzan.af.org.sa/sites/default/files/tafsir_27-07-1433.mp3
  • Imechapishwa: 23/05/2018