Allaah (Subhaanah) amesema:

وَإِن تُطِعْ أَكْثَرَ مَن فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ

“Na kama ukiwatii wengi walioko ulimwenguni, watakupoteza na njia ya Allaah.” (06:116)

Njia ya Allaah ni Qur-aan na Sunnah:

إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ هُمْ إِلَّا يَخْرُصُونَ

“Hawafuati isipokuwa dhana tu, na hawakuwa ila wenye kubuni uongo.” (06:116)

Watu hawa hawakufuata njia; Qur-aan na Sunnah; wamefuata dhana na matamanio. Ndio maana inazingatiwa kuwa ni katika neema kubwa ambayo mja muumini anaweza kupata yeye akawa ni mwenye kushikamana bara bara na Qur-aan na Sunnah mpaka wakati wa kufa. Hii ni neema kubwa kabisa. Watu wengi hawawezi mtihani huu. Watu wengi wamekhasirika kwa sababu ima hawajapatapo kupita katika njia iliyonyooka au wamepita juu yake kisha wakapinda. Mafanikio hayawi isipokuwa kwa kuendelea mpaka pale Allaah atapokufisha. Fuata Qur-aan na Sunnah mpaka wakati wa kufa. Haafidhw Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) ametaja katika kitabu “al-Bidaayah wan-Nihaayah” namna ambavyo shaytwaan alimjia Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) wakati alipokuwa anataka kukata roho na kumwambia:

“Nimekukosa, ee Ahmad.”

Anamaanisha kwamba hakufanikiwa kumpotosha. Wakati Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) aliposikia hivyo akasema:

“Bado.”

Bi maana roho haijatengana na kiwiwili. Pale ambapo roho itaachana na mwili ilihali bado ni mwenye kufuata Qur-aan na Sunnah ndipo Allaah atakuwa amekunusuru. Hapo ndipo Allaah atakuwa amekunusuru. Ina maana kwamba mtu asijiaminie. Usijiaminishe na vitimbi na hila za shaytwaan maadamu bado uko hai. Midhali bado uko hai usijiaminishe kutopata mwisho mbaya.

  • Mhusika: ´Allaamah Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab al-Wasswaabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ath-Thabaat ´alaa as-Swiraat al-Mustaqiym yakuun bil-´Ilm http://olamayemen.com/Dars-9998
  • Imechapishwa: 06/05/2018