Swali: Ni ipi hukumu kwa mwanamme kuvaa pete ya ndoa ya fedha?

Jibu: Kuvaa pete ya ndoa kwa wanamme na wanawake ni miongoni mwa vitu vilivyozuliwa. Pengine hata ikawa ni haramu kwa vile baadhi ya watu wanaamini kuwa kuvaa pete ya ndoa ni sababu inayofanya kubaki kwa yale mapenzi kati ya wanandoa. Kwa ajili hiyo nimemsikia baadhi ya wanandoa kila mmoja huandika jina la mwenzie. Inaonekana ni kama kwamba wanakusudia kudumisha mapenzi kati yao. Kitendo kama hicho ni aina fulani ya shirki kwa sababu wanaamini kuwa pete ya ndoa ni sababu inayodumisha mapenzi, kitu ambacho Allaah hakukifanya kuwa ni sababu ya mapenzi si kwa njia ya kikadiri wala ya kidini. Pete hii ina mafungamano yepi na mapenzi? Ni wanandoa wangapi wasiovaa pete ya ndoa wanawapenda wake zao kuliko wanavofanya wale wanandoa wenye kuvaa pete za ndoa! Ni wanandoa wangapi wenye kuvaa pete za ndoa wanaishi maisha ya magomvi na yasiyo na furaha! Kwa hivyo pete ya ndoa iliyoambatana na imani mbovu ni aina fulani ya shirki. Pasi na imani hiyo bado inakuwa nu kujifananisha na wasiokuwa waislamu. Kwa sababu pete za ndoa hizi zimetoka kwa manaswara. Kujengea juu ya haya ni lazima kwa muislamu kujiepusha na kila kitu kinachoidhuru dini yake.

Kuhusu mwanaume kuvaa pete ya fedha isiyokuwa pete ya ndoa, ni jambo lisilokuwa na ubaya. Inafaa kwa wanamme kuvaa pete ya fedha, na ni haramu kuvaa pete ya dhahabu. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhuma) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwona bwana mmoja mkononi mwake amevaa pete ya dhahabu, akaichukua na kuitupa na akasema: “Je, hivi kweli mmoja wenu anakusudia kuweka kaa la moto mkononi mwake?”[1]

[1] Muslim (2090).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (18/100)
  • Imechapishwa: 10/05/2021