Njia tatu za kufunga swawm ya ´Aashuuraa’

Swali: Kuna watu wanaosema kuwa kufunga siku moja pekee siku ya ´Aashuurah ndio Sunnah kwa sababu kitendo cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kinatangulia kabla ya maneno yake. Je, mtazamo huu ni sahihi?

Jibu: Hapana, si sahihi. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mwishoni mwa uhai wake:

“Nikibaki mpaka mwaka ujao basi nitafunga tarehe tisa na kumi.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… nitafunga siku kabla yake.”

 Katika upokezi mwingine imekuja:

“… na siku baada yake.”

Lakini hii ina udhaifu ndani yake. Maneno yake:

“Nikibaki mpaka mwaka ujao basi nitafunga tarehe tisa na kumi.”

inapatikana katika “as-Swahiyh” ya Muslim. Maneno yanatangulia kabla ya kitendo. Maneno ndio msingi. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaweza kusema jambo na huenda vilevile asilifanye kwa kutokuwa na uwezo. Anaweza kukokoteza kufunga, kama Dhul-Hijjah, na wala asiweze yeye kufunga kwa sababu ya kushughulika kwake na Da´wah, kueneza elimu, kuagiza majeshi na mengineyo. Sunnah inathibiti kwa maneno, vitendo na kulikubali jambo. ´Allaamah Ibn-ul-Qayyim amesema kuwa kuna njia tatu za kufunga:

Ya kwanza: Kufunga siku moja kabla yake na baada yake. Hili ndio bora zaidi. Huku ndani yake kuna kufunga siku tatu kwa mwezi.

Ya pili: Kufunga tarehe tisa na kumi.

Ya tatu: Kufunga tarehe kumi peke yake. Hili jambo ni sawa lakini hata hivyo limechukizwa. Mtu atakuwa ameafikiana na mayahudi katika jambo hili. Lakini hata hivyo halina neno.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Mutanawwi´ah (03) http://audio2.islamweb.net/lecturs/aalrrajhee/430/430.mp3
  • Imechapishwa: 03/04/2018