Nini maana ya Namsw na inahusu wanawake peke yao?

Swali: Imepokelewa katika Hadiyth Swahiyh:

“Allaah amewalaani wanawake wenye kuchanja wenzao na wenye kuchanjwa, wenye kunyoa wenzao nyusi (النَّمص) na wenye kunyolewa na wenye kutia mwanya meno yao na wenye kutiwa.”

Je, النَّمص imefungamana na nyusi peke yake au pia inahusu kutoa baadhi ya nywele za usoni? Je, mwanamme pia anaingia ndani ya makatazo haya au ni jambo linawahusu wanawake peke yao?

Jibu: Ni Hadiyth Swahiyh iliyopokelewa na al-Bukhaariy na Muslim. Wanachuoni wametofautiana juu ya neno hilo. Wako waliosema ni jambo maalum juu ya kunyoa na kuchonga nyusi. Hiyo ndio maana ya النَّمص. Wengine wakasema kuwa ni jambo linahusu nyusi na uso mzima. Wamesema ni kule kuondosha nywele zozote za usoni kukiwemo nywele za mashavuni na nyusi. Waliotajwa ni wanawake peke yao. Lakini mtu anaweza kusema kuwa ile sababu ni yenye kuenea. Hadiyth imetaja wanawake. Lakini hata hivyo sababu, ambayo ni kule kubadilisha na kuyafanya vibaya maumbile ya Allaah, ni yenye kuenea wote. Kwa hiyo si jambo maalum kwa wanawake. Hata kama Hadiyth imewazungumzia wao peke yake. Sababu – na Allaah ndiye mjuzi zaidi – ni kwa sababu wao ndio wenye mazowea na kupupia kufanya hivo kwa madai eti kwa kufanya hivo wanawapambia waume zao. Ndio maana Hadiyth ikawataja wao. Lakini kinachodhihiri ni kwamba ni hukumu kuwahusu wote. Kwa ajili hiyo kufanya chanjo mwilini ni kitendo cha haramu hata kwa wavulana. Hadiyth imesema:

“… wanawake wenye kuchanja… “

Lakini akifanya mwanamme pia ni haramu. Hivi ndivo yalivo masuala ya النَّمص. Dhahiri ni kwamba ni jambo la kuenea. Haifai kwa mwanamme kunyoa au kuchonga nyusi zake na vivyo hivyo nywele za mashavuni. Kwa sababu nywele zilizoko mashavuni zinazingatiwa ni ndevu pia. Ndani ya kamusi na kwengine imetajwa kwamba ndevu ni zile zenye kuota mashavuni na kwenye kidevu. Kwa hali yoyote khatari zaidi ni النَّمص inayohusiana na nyusi.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaad-Duruus https://binbaz.org.sa/fatwas/3694/%D8%AD%D9%83%D9%85-%D8%A7%D9%84%D9%86%D9%85%D8%B5-%D9%81%D9%8A-%D8%AD%D9%82-%D8%A7%D9%84%D9%86%D8%B3%D8%A7%D8%A1-%D9%88%D8%A7%D9%84%D8%B1%D8%AC%D8%A7%D9%84
  • Imechapishwa: 19/05/2020