Nia mbalimbali za kusomea elimu za kidunia


Swali: Kauli ya Allaah (Ta´ala):

قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ

“Je, wanalingana sawa wale wanaouja na wale wasiojua?” (39:09)

Na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Wanachuoni ndio warithi wa Mitume (´alayhims-Swalaat was-Salaam).”

Je, makusudio ni wanachuoni wa utabibu, kemia au wasiokuwa hao? Au makusudio ni wanachuoni wa Shari´ah?

Jibu: Makusudio kwa makubaliano ya wanachuoni wote ni ma´ulamaa wa Shari´ah, wanaochukua kutoka katika Kitabu na Sunnah. Wana fadhila kubwa na kheri nyingi. Ama kuhusiana na elimu ya udaktari, uhandisi na elimu zingine za dunia zinazofafana na hizo, ni elimu ambazo watu wao hukumu yao ni kiasi cha makusudio yao. Yule ambaye atajifunza uhandisi au udaktari ili awanufaishe Waislamu dhidi ya maadui wao, huyu ni mwenye kupewa ujira kwa kiasi cha nia yake. Hali kadhalika, kwa yule mwenye kusomea uanaskari, vita ili aje kuwanufaisha Waislamu, au akasomea uanajeshi ili makusudio yake ni kuwanufaisha Waislamu, huyu ni mwenye ujira na hukumu yake itakuwa kama ya wanachuoni wa Shari´ah. Ujira itategemea nia yake. Ama mwenye kusomea elimu ya dunia kwa makusudio ya kupata dunia ili aweze kula, au kupata kazi na kuishi, hili limeruhusiwa na hana juu yake kitu. Kwa kuwa Shari´ah imeamrisha kutafuta riziki. Lakini mtu huyu hawi kama yule aliyejifunza ili aweze kula pato la Halali na ajitosheleze na kuwaomba watu au awanufaishe Waislamu dhidi ya maadui wao, nia inatofautiana. Mwenye kujifunza kwa nia nzuri atakuwa ni mwenye ujira. Na mwenye kujifunza nayo ili ajiepushe na Haramu na achume pato la Halali, ni mwenye ujira. Na mwenye kujifunza nayo, hana makusudio yoyote ila tu ili apate kuishi, kula na kunywa, na makusudio yake sio kuwanufaisha Waislamu, yeye kajifunza nayo kwa maslahi ya kidunia tu, huyu kwake itakuwa inaruhusiwa tu.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.alharamain.gov.sa/index.cfm?do=cms.scholarallsubjects&schid=8177
  • Imechapishwa: 20/01/2018