Ni wajibu kwa anayetaka kusujudu sijda ya kusahau kusoma Tashahhud nyingine?

Swali: Niliwahi Rak´ah mbili kwenye swalah ya mkusanyiko na pambizoni mwangu kulikuweko watu watatu ambao waliwahi Rak´ah tatu. Lakini nikatoa salamu pamoja nao kwa kusahau. Lakini baadaye nikakumbuka kuwa kumebaki Rak´ah moja ambapo nikainuka na kuiswali na kutoa salamu. Wakanambia kwamba nisujudu sijda ya kusahau. Nikawauliza nisujudu vipi ambapo wakanambia kuwa nisoma Tashahhud mara ya pili kisha ndio nisujudu sijda ya kusahau halafu nitoe salamu, jambo ambalo nililifanya. Je, nilipatia kwa kufanya hivo?

Jibu: Uhakika wa mambo ni kwamba ulichokifanya si cha sawa. Kwa sababu ulipotoa salamu pamoja nao baada ya kuswali Rak´ah moja na ulikuwa unadaiwa kuswali Rak´ah mbili, umekuwa mwenye kutoa salamu kabla ya swalah kukamilika. Kwa aliyetoa salamu kabla ya swalah kumalizika kisha ima akakumbuka mwenyewe au akakumbushwa aikamilishe lililo la wajibu kwake ni yeye kuikamilisha swalah yake, kisha atoe salamu halafu asujudu sijda mbili za kusahau kisha atoe salamu. Si wajibu kwake – kama alivoambiwa na watu hawa – kwamba asome Tashahhud, kisha atoe  salamu halafu asujudu sijda ya kusahau. Jambo hili halina msingi wowote. Kwa sababu mara ya kwanza ameshasoma Tashahhud na hivyo hakuna haja ya kuirudi.

Lililo la wajibu kwa yule ambaye ametoa salamu kabla ya swalah kukamilika – ni mamoja ni ambaye amekuja kuchelewa na akasalimu pamoja na imamu au wale anaoswali naye, kama ilivyo katika hali hii, anayeswali peke yake au imamu – aswali kile kilichobaki kwake kwanza kisha ndio atoe salamu. Halafu baada ya hapo asujudu sijda mbili za kusahau na atoe salamu. Hii ndio hukumu ya Kishari´ah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (12) http://binothaimeen.net/content/6765
  • Imechapishwa: 09/01/2021