Ni wajibu kuweka nia usiku kwa ajili ya kufunga Ramadhaan

Swali: Je, uwekaji wa nia ya Ramadhaan unakuwa katika sehemu ya usiku au hata ya mchana? Kwa mfano mtu ameambiwa wakati wa dhuhaa ya kwamba leo ni Ramadhaan alipe siku hiyo au asilipe?

Jibu: Ni wajibu kuweka nia ya kufunga mwezi wa Ramadhaan usiku kabla ya alfajiri. Haikubaliki kuanza kuweka nia ya kufunga mchana. Yule atakayejua wakati wa dhuhaa ya kwamba leo ni Ramadhaan na akanuia kufunga basi ni wajibu kwake kujizuia na kula na kunywa mpaka wakati wa kuzama jua. Hata hivyo ni lazima kuilipa siku hiyo. Ibn ´Umar amepokea kutoka kwa Hafswah (Radhiya Allaahu ´anhum) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule asiyejumuisha kufunga kabla ya alfajiri swawm yake si sahihi.”[1]

Ameipokea Imaam Ahmad, waandishi wa “as-Sunan”, Ibn Khuzaymah, Ibn Hibbaan ambaye ameisahihisha kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hii ni kuhusu swawm ya faradhi.

Kuhusu swawm ya Sunnah inajuzu kuweka nia ya kufunga mchana ikiwa mtu bado hajala, hajanywa na wala hajafanya jimaa baada ya alfajiri. Kwa kuwa imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupitia Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba siku moja aliingia wakati wa dhuhaa akasema:

“Je, kuna chochote?” Akamjibu: “Hapana.” Akasema: “Basi mimi nafunga.”[2]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

[1] Ahmad (06/287), Abu Daawuud (02/823-824), at-Tirmidhiy (03/108) na wengineo.

[2] Ahmad (06/49/207), Muslim (02/808-809), Abu Daawuud (02/824-825) na wengineo.

  • Mhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (10/244-245)
  • Imechapishwa: 10/06/2017