Ni vipi nitajua mtihani uliyonipata ni jaribio tu au ni adhabu ya Allaah?

Swali: Pindi anapopewa mtihani kwa ugonjwa au msiba katika nafsi yake au mali – ni vipi atajua jambo hilo kuwa ni jaribio, mtihani au ghadhabu kutoka kwa Allaah?

Jibu: Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) huwapa mtihani waja Wake kwa mazuri, madhara, magumu na ustawi. Vilevile anaweza kuwapa majaribio yao ili kuzinyanyua daraja zao, kunyanyua utajo wao na kuyaongeza matendo yao mema. Hivo ndivo wanavofanyiwa Manabii na Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) na wema katika waja wa Allaah. Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu wenye mitihani mizito ni Mitume, kisha mfano wao, kisha mfano wao.”

Wakati mwingine hufanya hivo (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa sababu ya maasi na madhambi. Katika hali hiyo adhabu inakuwa ni yenye kuja kwa haraka. Amesema (Subhaanah):

وَمَا أَصَابَكُم مِّن مُّصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ وَيَعْفُو عَن كَثِيرٍ

“Haukupateni katika msiba wowote basi ni kwa sababu ya yale yaliyochuma mikono yenu na anasamehe mengi.”[1]

Mara nyingi kwa mtu ni hali ya mapungufu na kutosimama kwa yale mambo ya wajibu. Kwa hivyo ile misiba inayompata ni kwa sababu ya madhambi na mapungufu yake juu ya amri za Allaah.

Akipewa jaribio mmoja katika waja wema wa Allaah kwa kitu katika maradhi au mfano wake, basi jambo hilo linakuwa ni katika ile aina ya majaribio ya Manabii na Mitume kwa lengo la kunyanyuliwa ngazi na kuongezewa thawabu. Lengo lingine ni ili yeye awe ni kiigizo kwa wengine katika kusubiri na kutaraji malipo kutoka kwa Allaah.

Kwa kifupi ni kwamba mtihani unaweza kuwa na maana ya kunyanyuliwa daraja na kuongezewa thawabu. Hivo ndivo Allaah huwafanyia Mitume na baadhi ya wema. Mtihani unaweza pia kuwa na maana ya kufutiwa makosa. Amesema (Ta´ala):

مَن يَعْمَلْ سُوءًا يُجْزَ بِهِ

“Yeyote atakayefanya uovu atalipwa kwayo.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) amesema:

“Muislamu hapatwi na kutaabika, uzito, maradhi, huzuni, maudhi, dhiki mpaka ule mwiba unaomchoma isipokuwa Allaah humfutia dhambi zake kwayo.”

Vilevile amesema  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule ambaye Allaah anamtakia kheri basi humwonjesha mtihani.”

Mtihani huo vilevile unaweza kuwa na maana ya adhabu iliyokuja haraka kwa sababu ya maasi na kutokimbilia kufanya tawbah. Imepokelewa katika Hadiyth kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) kwamba amesema:

“Allaah anapomtakia mja Wake kheri, basi humharakishia adhabu duniani, na anapomtakia mja Wake shari, humcheleweshea adhabu ya dhambi yake mpaka amlipe kwayo siku ya Qiyaamah.”

Ameipokea at-Tirmidhiy na ameifanya kuwa nzuri.

[1] 42:30

[2] 04:123

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/371)
  • Imechapishwa: 14/03/2020