Ni vipi mfungaji atakata swawm akiwa ndani ya ndege?

Swali: Inafaa kwa mfungaji kukata swawm akiwa ndani ya ndege na kwa mujibu wa saa na simu alionayo jua limeshazama na kwa mujibu vilevile wa nchi alio karibu nayo? Lakini hata hivyo tambua kuwa bado anaona jua kwa sababu ya upaaji wa ndege. Ni ipi hukumu ikiwa atafungua kwa nchi hiyo kisha ndege ilipotua transiti akaona jua?

Jibu: Ikiwa mfungaji yuko ndani ya ndege na akaona jua limezama kwa mujibu wa saa na simu na kwa mujibu vilevile wa nchi alio karibu nayo lakini hata hivyo akawa anaona jua kwa sababu ya upaaji wa ndege, haifai kwake kukata swawm. Allaah (Ta´ala) amesema:

“Kisha timizeni swawm mpaka usiku.”[1]

Lengo hili halijahakikishwa kwake midhali bado anaona jua. Ama ikiwa atakata swawm na nchi fulani baada ya kuingia usiku wa nchi hiyo na ndege ikatua transiti halafu akaona jua, ataendelea katika hali ya kula. Kwa kuwa ana hukumu moja na nchi ile ambayo punde ameitoka ambayo usiku umeingia akiwa ndani yake.

[1] 02:187

  • Mhusika: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (10/136-137)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Imechapishwa: 30/05/2017