Ni Sunnah kuswali Rak´ah mbili baada ya ´Aswr

3174- Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) haachi Rak´ah mbili kabla ya Fajr na Rak´ah mbili baada ya ´Aswr.

Ameipokea Ibn Abiy Shaybah katika ”al-Muswannaf” (2/352): ´Affaan ametuhadithia: Abu ´Awaanah ametuhadithia: Ibraahiym bin Muhammad bin al-Muntashir ametuhadithia, kutoka kwa baba yangu ambaye alikuwa akiswali Rak´ah mbili baada ya ´Aswr. Wakati alipoulizwa akasema:

”Nisingeziswali isipokuwa ni kwa sababu nilimuona Masruuq akiziswali, pamoja na kwamba alikuwa ni mtu mwaminifu. Lakini nikamuuliza ´Aaishah kuhusu jambo hilo ambapo akasema:

”Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) haachi Rak´ah mbili kabla ya Fajr na Rak´ah mbili baada ya ´Aswr.”

Miongoni mwa makosa yaliyoenea katika vitabu vya Fiqh ni pale wanapokataza Rak´ah mbili hizi bali na kutozitaja miongoni mwa jumla ya Sunnah za Rawaatib, pamoja na kwamba zimethibiti kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akidumu kwazo kama ambavyo alikuwa akidumu kuswali Rak´ah mbili za kabla ya Fajr. Hakuna dalili yoyote inayoonyesha kuwa zimefutwa au kwamba ni mambo maalum kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pekee. Ni vipi iwe hivyo ilihali mjuzi zaidi wa watu alikuwa akizihifadhi, naye si mwengine ni mama wa waumini ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa), na Maswahabah na Salaf wengine walioafikiana naye?

Aidha inatakiwa kutambulika kwamba zile Hadiyth zilizokuja kwa jumla zinazokataza kuswali baada ya ´Aswr zimekuja kwa njia iliyofungamana kwa Hadiyth zengine Swahiyh ambazo zimesema wazi kwamba inafaa kuswali midhali jua bado halijakuwa manjano. Moja katika Hadiyth hizo ni ile ya ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) inayosema:

”Msiswali baada ya ´Aswr isipokuwa mkiswali jua liwe limeshainuka.”

Hadiyth ni Swahiyh na imepokelewa kwa njia nyingi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (7/1/528)