Ni nani na kwa njia gani mtawala anasimamishiwa hoja?

Swali: Kuhusu kumsimamia hoja mtawala. Nini maana yake na ni vipi mtu anafanya hivo na nani mwenye kufanya?

Jibu: Anayefanya hivo ni wanachuoni. Hilo linafanyika kwa Kitabu cha Allaah na Hadiyth za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na matendo ya Salaf. Kipi zaidi ulichouliza?

Swali: Nini maana ya kusimamisha hoja?

Jibu: Ni kama alivosema Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah):

“Elimu ni “Allaah amesema, Mtume Wake amesema, Maswahabah wake wamesema… “”

Hoja ni kunukuu yale yaliyosemwa na Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Si zaidi ya hivo.

Swali: Haya yanafanyika kwa njia ya moja kwa moja au kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja?

Jibu: Si lazima haya yafanyike kwa njia ya moja kwa moja. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipowalingania katika Uislamu wafalme makafiri hakufanya hivo kwa njia ya moja kwa moja. Aliwatumia barua. Wakati mwingine aliwatumia mjumbe. Kwa hiyo si jambo la lazima hoja isimame kwa njia ya moja kwa moja. Hilo linaweza kufanyika kwa njia ya mkati na kati. Endapo hivi sasa tutawasiliana na yule ambaye tunataka kumsimamishia hoja, tutafanya hivo kwa kutanguliza yale aliyosema Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Sambamba na hilo kuna miaka elfu moja na mia nne kati yetu sisi na Mtume aliyetufikishia Shari´ah ya Allaah. Kwa hiyo kuko ukatikati katika kumfikishia mtu hoja, ijapo mtu atafanya hivo kwa njia ya moja kwa moja. Jambo muhimu mtu afikiwe na hoja pasi na kujali ni kwa njia ya yule mjumbe aliyemwendea, kama ilivyokuja katika Hadiyth Swahiyh:

“Jihaad bora ni neno la haki mbele ya mtawala dhalimu.”

Lakini endapo mtu atamtumia barua na akambainishia masuala hayo kwa dalili za Qur-aan na Sunnah, basi itakuwa imebainikia hoja.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Hudaa wan-Nuur (468)
  • Imechapishwa: 07/06/2021