Swali: Ni mambo gani yanayomfunguza mfungaji?

Jibu: Mambo yanayomfunguza mfungaji ni saba:

1- Jimaa. Mfungaji akitenda tendo la ndoa mchana wa Ramadhaan basi ni lazima kwake kuilipa siku hiyo pamoja vilevile na kutoa kafara ambayo ni kuachia mtumwa huru, asipopata basi afunge miezi miwili mfululizo, asipoweza basi atatakiwa kuwalisha masikini sitini. Ima awalishe au ampe kila mmoja wao robo Swaa´ ya ngano au mchele. Imependekezwa vilevile pamoja na vitu hivyo awape kitoweo kama nyama au kitu kingine.

2- Kutoa manii ima kwa kutazama, punyeto, jimaa, kubusu au kukumbatia.

3- Kula au kunywa. Ni mamoja kinywaji hicho kiwe chenye manufaa au chenye madhara kama ilivyo sigara.

4- Kudungwa sindano ambayo inachukua nafasi ya chakula. Kwa kuwa sindano kama hii ina maana moja kama ya kula na kunywa. Kuhusu sindano isiyokuwa ya chakula haiharibu swawm. Ni mamoja inadungwa kwenye misuli au kwenye mifupa ya kupitisha damu. Ni mamoja mtu akahisi ladha yake kooni au asihisi.

5- Kutokwa na damu ya hedhi na nifasi.

6- Kutoa damu kwa kufanyiwa chuku na mfano wake. Kama kuchotwa damu nyingi ambayo inaudhoofisha mwili kama ilivyo inapokuja katika kuumikwa. Kuhusu kutokwa na damu kama kwenye pua, kung´oa jino na mfano wake hakuharibu swawm. Kwa sababu huku sio kuumikwa na wala hakuleti maana hiyo.

7- Kujitapisha. Mtu kutapika kwa kutopenda kwake hakufunguzi.

Tunapenda vilevile kuzindua ya kwamba swawm ya mfungaji haiharibiki endapo atafanya kitu katika mambo yanayofunguza kwa kusahau, kutokujua au kulazimishwa. Iwapo mfungaji atakula na kunywa kwa kusahau swawm yake haiharibiki. Endapo vilevile atakula au atakunywa kwa kuamini kuwa jua limeshazama au ya kwamba alfajiri haijaingia swawm yake haiharibiki. Kwa kuwa ni mjinga. Iwapo vilevile atalala na kutokwa na manii swawm yake haiharibiki kwa kuwa hakufanya kwa kupenda kwake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (19/201-202)
  • Imechapishwa: 09/06/2017