Ni lipi la kufanya kwa wale walio mbele ya anayetaka kukata roho?

Swali: Aliyekaa afanye nini mbele ya ambaye anataka kukata roho? Kumsomea “Yaa Siyn” ambaye anataka kukata roho ni jambo limethibiti katika Sunnah au halikuthibiti?

Jibu: Kumtembelea mgonjwa ni haki ya muislamu kwa muislamu mwenzie. Inatakiwa kwa yule anayemtembelea mgonjwa amkumbushe kutubia, ule wasia ambao ni wajibu kwake na autumie muda wake kumdhukuru Allaah (´Azza wa Jall). Hakika mgonjwa ni mwenye haja kwa kitu kama hichi.

Mtu atapoyakinisha kuwa mauti yamemjia, basi anatakiwa amlakinie “Laa ilaaha illa Allaah”. Hivo ndivyo alivyoamrisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amtajie Allaah kwa sauti atayoisikia mpaka akumbuke na amdhukuru Allaah. Wanachuoni wamesema:

“Haifai kumuamrisha kufanya hivo. Huenda akawa na dhiki kifuani mwake na akawa katika hali ngumu ambapo matokeo yake akakataa kutamka shahaadah. Hatimaye aje kupata mwisho mbaya. Badala yake anatakiwa kumkumbusha kimatendo kwa njia ya kumtajia Dhikr mpaka aweze kuisema. Pale atapotamka shahaadah tu basi anyamaze na wala asimzungumzishe baada ya hapo. Lengo ni ili maneno yake ya mwisho kutamka iwe ni shahaadah. Endapo itatokea akatamka [maneno mengine] basi amlakinishe tena kwa mara ya pili ili maneno yake ya mwisho iwe ni shahaadah.”

Kuhusu kumsomea “Yaa Siyn” ambaye anataka kukata roho wanachuoni
wengi wanaonelea kuwa ni Sunnah. Hilo ni kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Wasomeeni maiti wenu “Yaa Siyn.”” Ahmad (04/257) na Abuu Daawuud (3121).

Lakini hata hivyo kuna wanachuoni wameitia dosari na kuidhoofisha Hadiyth hii.

Kwa hiyo kusoma Suurah hii kwa wale walioisahihisha itahesabika ni Sunnah. Kuhusu wale walioidhoofisha itahesabika si Sunnah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/71-72)
  • Imechapishwa: 17/06/2017