Ni lini mtu anazingatiwa ni msafiri kwa mtazamo wa al-Albaaniy

Swali 327: Ni lini mtu anafupisha swalah katika safari?

Jibu: Hakuna andiko la wazi kutoka katika Qur-aan na Hadiyth linaloweza kuzingatiwa kuwa ni andiko la kukata linalotambulika juu ya masafa ambayo yanazingatiwa msafiri kufupisha swalah au safiri ambayo inafaa kwa msafiri kufupisha swalah yake. Kilichopo ni maoni yaliyopewa nguvu peke yake. Sisi tuko pamoja na wale waliochagua kwamba safari ni safari ambayo inaandamwa na hukumu za safari na msafiri. Jambo hili limechukuliwa kwa mfano kutoka katika maneno Yake (Ta´ala):

فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu au yuko safarini, hivyo basi akamilishe idadi katika siku nyinginezo.”[1]

Kama ambavyo Allaah (´Azza wa Jall) katika Aayah tukufu hii ametaja maradhi kwa njia ya kuachia ndivo alivotaja safari kwa kuachia. Vovyote itavokuwa safari – ni mamoja iwe ndefu au fupi – basi hiyo ni safari ambayo inaandamwa na hukumu zake. Hakuangaliwi masafa baada ya hapo. Maoni haya ndio chaguo la Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah katika kijitabu chake maalum kuhusu hukumu za safari.

Kwa hivyo anapotoka msafiri katika mji wake kunathibiti juu yake hukumu za msafiri. Anapotua katika mji aliokuwa anaulenga bado anaendelea kuwa msafiri pasi na kujali atakaa siku nyingi au ndogo muda wa kuwa hajanuia kubaki huko. Lakini ikiwa hajanuia kubaki hapo na wakati huohuo anaiambiza nafsi yake kuwa leo ama kesho nitasafiri, vovyote utavorefuka muda ataokaa nao katika mji aliouendea, bado ni mwenye kuendelea kuwa msafiri.

Imethibiti kwamba Maswahabah wakati alipotoka kwenda kupambana Jihaad katika njia ya Allaah upande wa Khuraasaan waliteremkiwa na theluthi na wakapotewa na njia ya kurudi katika mji wao. Matokeo yake wakarefukiwa na miezi sita ambapo walikuwa wakifupisha swalah.

[1] 02:184

  • Mhusika: Imama Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Mar´ah al-Muslimah, uk. 123
  • Imechapishwa: 24/03/2020