Ni lazima wakati wa kuomba du´aa kuikariri mara tatu?

Swali: Moja miongoni mwa sharti za du´aa ni kuikariri mara tatu. Khatwiyb siku ya ijumaa alisoma du´aa mara moja tu baada ya Khutbah ya msikitini. Je, inafaa kufanya hivo? Tunaomba kuwekewa wazi.

Jibu: Mambo si kama alivyofahamu ndugu huyu ya kwamba miongoni mwa sharti za du´aa ikaririwe mara tatu. Hii ni miongoni mwa adabu ambayo sio sharti. Inafaa kwa mtu akamuomba Allaah (Ta´ala) mara moja. Kwa msemo mwingine ni kwamba asikariri ile jumla aloomba kwayo. Kule kukariri ni kwa minajili ya adabu na si kwa minajili ya sharti.

Lakini ni muhimu itambulike kwamba miongoni mwa sharti za du´aa ni kwamba mtu awe muumini kwa yule anayemuomba na kwamba ni muweza wa kumuitikia maombi yake.

Kadhalika miongoni mwa adabu ambazo ni muhimu sana ni yeye kujiepusha na haramu katika vyakula, vinywaji na mavazi. Kwani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtaja mtu ambaye amerefusha safari akiwa na nywele timtim na amejaa vumbi huku akinyanyua mikono yake mbinguni na akisema: “Ee Mola wangu! Ee Mola wangu!” Yote haya ni miongoni mwa sababu za du´aa kuitikiwa. Anaendelea kusimulia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Chakula chake ni haramu, mavazi yake ni haramu na amelishwa haramu – vipi atajibiwa?”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaeleza kwamba mtu huyu kuitikiwa du´aa yake ni jambo liko mbali ambaye kumepatikana kwake sababu za kuitikiwa du´aa kwa sababu ya kuwepo vikwazo hivi vyenye nguvu; amelishwa haramu na kuvishwa haramu.

Kwa hali yoyote kitendo cha Khatwiyb cha yeye kuomba du´aa mara moja tu katikati ya Khutbah hakuna ubaya.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (02) http://binothaimeen.net/content/6634
  • Imechapishwa: 09/03/2019