Swali: Katika mji ninapoishi wakati anapokufa mtu wanakusanyika ndugu, marafiki na jamaa zake kwa ajili ya kumsindikiza, kumzika, kuwapa pole ndugu zake na kuwapa misaada ya kipesa ili familia ya wafiliwa waajiri wapishi kwa ajili ya kuwaandalia chakula wageni waliokuja kuzika. Mambo haya hutendeka kuanzia siku tatu mpaka siku saba. Wanaamini kuwa kitendo hichi kinafanya uhusiano baina yao kuwa na nguvu na kuwafanya wakapendana. Vilevile wanaamini kuwa chakula hichi ni swadaqah yenye kukubaliwa juu ya roho ya maiti ambacho kinaliwa na tajiri na masikini, mdogo na mkubwa, mwanamke na muhitaji. Je, kitendo hichi ni sahihi? Je, ni sahihi kwa muislamu kula chakula hichi na kuhudhuria mfano wa kikao hichi?

Jibu: Kitendo hichi si sahihi. Kitendo hichi – nikimaanisha kukusanya swadaqah na matanga yaliyotajwa – si sahihi. Kuhusu marafiki na ndugu kukusanyika kwa ajili ya kumsindikiza maiti na kutoka na jeneza lake ni kitu kisichokuwa na ubaya wowote. Ni Sunnah. Hapana shaka kwamba kumsindikiza maiti ni katika Sunnah na khaswa akiwa na haki kama ya udugu, urafiki, kujifunza na mengineyo.

Ama matanga haya yanayoenda kwa muda wa siku tatu, siku saba au siku arubaini ni miongoni mwa Bid´ah ambazo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza na akautahadharisha Ummah wake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuyafanya, hayakufanywa na Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anh) wala as-Salaf as-Swaalih. Wao ni wenye pupa zaidi kuliko sisi katika kheri.

Kile tunachoweza kuwanasihi ndugu zetu katika nchi hii inayofanya haya yaliyotajwa na muulizaji waache kujichosha nafsi zao na kuiharibu mali katika mambo kama haya ambayo hayana nafasi yoyote katika Shari´ah. Ikiwa kuna mmoja katika ndugu zake anayetaka kumfaa basi amtolee swadaqah kwa njia ya siri na sio kwa njia kama hii inayotangazwa na watu hawa.

Swali: Ni sawa kwa muislamu kula chakula kama hichi na kuhudhuria kikao hichi?

Jibu: Hapana. Haitakiwi kwa muislamu kuhudhuria mfano wa matanga kama haya. Bali imechukizwa kwake kufanya hivo au imeharamishwa. Kwa sababu kufanya hivi ni kuipa nguvu Bid´ah. Mwenye kuipa nguvu Bid´ah ni kama yule anayeifanya. Kwa ajili hiyo tunawatahadharisha ndugu zetu kuhudhuria mfano wa matanga kama haya, kuyapa nguvu na kuyakubali. Bali ni lazima kwa muislamu kuyakemea mambo haya.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (06) http://binothaimeen.net/content/6695
  • Imechapishwa: 04/11/2020