Swali: Je, mtu analipa swalah anapoiacha kwa makusudi anapomwongoza Allaah kutubia ni mamoja kile alichokiacha ni kipindi kimoja cha swalah au ni vingi?

Jibu: Haimlazimu kulipa akiacha kwa makusudi kutokana na maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Kwa sababu kuiacha kwa makusudi kunamtoa nje ya mzunguko wa Uislamu na kumfanya ni katika makafiri. Kafiri halipi yale aliyoyaacha katika kipindi cha ukafiri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

 “Baina ya mtu na shirki na ukafiri ni kuacha swalah.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ahadi iliopo kati yetu sisi na wao [makafiri] ni swalah. Hivyo basi, yule mwenye kuiacha amekufuru.”

Amepokea Imaam Ahmad na watunzi wa as-Sunan kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kupitia kwa Buraydah bin al-Huswayb (Radhiya Allaahu ´anh).

Isitoshe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wale makafiri waliosilimu hakuwaamrisha kulipa yale waliyoacha. Vivyo hivyo Maswahabah wake (Radhiya Allaahu ´anhum) hakuwaamrisha wenye kuritadi kulipa waliyoyacha pindi waliporudi katika Uislamu.

Yule ambaye ameacha swalah kusudi bila kupinga uwajibu wake akilipa hapana neno. Kufanya hivo ni kuchukua tahadhari na kutoka nje ya tofauti kwa wale wanaosema kuwa sio kafiri asipopinga uwajibu wake. Wanazuoni wengi ni wenye kuonelea hivo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/312)
  • Imechapishwa: 18/09/2021