Ni kweli Ahmad al-Khaliyliy anataka umoja wa waislamu?

Mwandishi al-Khaliyliy analingania umoja kwa maneno yake tu kisha anayavunja madai yake hayo kwa vitendo vyake. Amefanya hayo katika kitabu chake hichi – Haqq-ud-Daamigh – ambacho amekusanya baina ya vitu vyenye kujigonga. Upambanuzi wake ni kama ifuatavyo:

1- Mwandishi al-Khaliyliy amehukumu ya kwamba muislamu mtenda dhambi kubwa atadumu Motoni milele. Anaitakidi hivo, analithibitisha na kulingania kwalo na kusema kwamba hayo ndio madhehebu ya Ahl-ul-Haqq wal-Istiqaamah – Ibaadhiyyah – ambao anadai kuwa wanachukua dalili kutoka katika Qur-aan na Hadiyth zilizothibiti na wala hawazitangulizi akili juu yake kama wanavyofanya Mu´tazilah.

Je, huyu analingania katika kutaka kuleta umoja wa waislamu au analingania katika kuufarikisha na kuutawanyisha? Je, katika Ummah kuna ambaye amekingwa na kukosea mbali na Mitume na Manabii? Kuko wapi kuvumiliana ambako kipote chako wanasifika nako, kama ulivyodai. Mwandishi amesema katika ”Sentesi ya tatu”:

”Miongoni mwa mambo ambayo Ibaadhiyyah wanasifika nayo ni kuvumiliana katika kutangamana na mapote mengine ya Ummah kwa vile hawakufanya ujasiri wa kumtoa yeyote katika Uislamu na kumkatia kuwa na uhusiano na Ummah huu midhali mtu huyo anaamini shahaadah mbili.”

Mnamkatia vipi kuwa na uhusiano na Ummah huu ambaye anaamini shahaadah mbili ilihali mnamhukumu kudumu Motoni milele eti kwa sababu tu amefanya baadhi ya maasi? Maoni yenu haya yanaenda kinyume na maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehe kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[1]

Vilevile yanaenda kinyume na yale yaliyothibiti katika ”as-Swahiyh” kupitia kwa Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakuna mja atayesema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` kisha akafa juu ya hilo isipokuwa ataingia Peponi.” Nikasema: ”Hata kama atazini na kuiba?” Nikakariri hivo mara tatu ambapo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mara ya tatu: ”Amedhalilika Abu Dharr!” Abu Dharr akatoka akisema: ”Amedhalilika Abu Dharr!.”

Maana ya Hadiyth ni kwamba atayekufa juu ya Tawhiyd pasi na kumshirikisha Allaah hata kama atakuwa amefanya dhambi kubwa, kama kuzini na kuiba, hatodumishwa Motoni milele. Mwisho wake itakuwa Peponi baada ya kusafishwa na dhambi zake endapo Allaah hatomsamehe pale mwanzoni. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wameafikiana juu ya hilo kutokana na dalili hizi. Hakuna atakayedumishwa Motoni milele isipokuwa kafiri, mshirikina aliyefanya shirki kubwa yenye kumtoa katika Uislamu na mnafiki mwenye unafiki unaohusiana na ´Aqiydah ambaye anadhihirisha Uislamu na anaficha ukafiri. Tutayajadili mambo haya wakati tunapoyazungumzia. Mwandishi ameyawekea mlango maalum katika kitabu chake hichi.

[1] 04:116

  • Mhusika: ´Allaamah ´Aliy bin Naaswir al-Faqiyhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd al-Qawiym, uk. 19-20
  • Imechapishwa: 13/01/2017