Shaykh al-Albaaniy amejengea hoja upokezi hii kutoka kwa Ibn ´Abbaas[1] (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Vivyo hivyo wanazuoni wengine wamekubali upokezi huu ijapo katika cheni ya wapokezi wake kuna hili na lile. Hata hivyo, wameikubali kwa sababu inaafikiana na maandiko mengi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Kumtukana muislamu ni dhambi nzito na kumpiga vita ni ukafiri.”[2]

Pamoja na hivyo, kumpiga vita muislamu hakumtoi muislamu nje ya Uislamu. Amesema (Ta´ala):

وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا ۖ فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّـهِ ۚ فَإِن فَاءَتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا ۖ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

“Ikiwa makundi mawili ya waumini yatapigana, basi suluhisheni baina yao. Lakini mojawapo likikandamiza jengine, basi piganeni na ambalo linakandamiza mpaka lielemee katika amri ya Allaah. Likishaelemea, basi suluhisheni kati yao kwa uadilifu na tendeni haki. Kwani hakika Allaah anawapenda wanaotenda haki. Hakika waumini ni ndugu, hivyo basi suluhisheni kati ya ndugu zenu na mcheni Allaah ili mpate kurehemewa.”[3]

Lakini ilipokuwa jambo hili haliwaridhishi watu hawa waliopewa mtihani wa kukufurisha, ndipo wakaanza kusema:

“Upokezi huu si wenye kukubaliwa. Haukusihi kutoka kwa Ibn ´Abbaas.”

Ni vipi haukusihi ilihali umekubaliwa na wale ambao ni wakubwa zaidi, wabora na wajuzi zaidi wa Hadiyth kuliko nyinyi? Ni vipi mtasema kuwa hamuikubali?

Tumetoshelezwa na wanazuoni wakubwa kama vile Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah, Ibn-ul-Qayyim na wengineo wameikubali, wameizungumza na kuifikisha. Upokezi huo ni sahihi!

Hebu tukadirie kuwa haikuthibiti kutoka kwa Ibn ´Abbaas. Tuko na maandiko mengine yanayojulisha kwamba neno “ukafiri” linaweza kutumika na kusikusudiwe kwamba mtu ametoka nje ya dini. Mfano wa hilo ni kama ilivyotajwa katika Aayah tukufu. Mfano mwingine ni maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mambo mawili kwa watu ni kufuru; kutukaniana nasabu na kuomboleza juu ya maiti.”[4]

Hapana shaka yoyote kwamba mambo haya mawili hayamtoi mtu nje ya Uislamu.

Lakini uchache wa elimu na uelewa wa misingi ya Shari´ah ilioenea – kama alivosema Shaykh al-Albaaniy mwanzoni mwa maneno yake – ndio yanayosababisha upotofu huu.

Mtu anatakiwa kuongeza jambo jengine juu ya hayo; makusudio mabaya yanayopelekea katika ufahamu mbaya. Kama mtu anatak kitu kibaya, hilo litapelelekea ufahamu wake kwenda katika lile analolitaka kisha ayakengeusha maandiko kutokana na makusudio yake. Miongoni mwa misingi ya wanazuoni ni:

“Tafuta dalili kisha ndio amini.”

Mtu asiamini kisha ndio akajengea dalili. Huu ni upotofu. Sababu ya [upotofu wa kukufurisha] ni mambo matatu:

1 – Uchache wa elimu ya Shari´ah.

2 – Uchache wa uelewa juu ya misingi ya Shari´ah ilioenea.

3 – Ufahamu mbaya uliojengeka juu ya makusudio mabaya.

[1] Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

” وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio makafiri.” (05:44)

Ibn ´Abbaas amesema:

”Sio ule ukafiri wanaofikiri.”

”Sio ule ukafiri unaomtoa mtu nje ya dini. Ni ukafiri mdogo.”

“Ni ukafiri, lakini si kama kutomwamini Allaah na Qiyaamha.” (Tazama “ad-Durr al-Manthuur” (5/323-326) ya Imaam as-Suyuutwiy))

[2] al-Bukhaariy (48) na Muslim (64).

[3] 49:9-10

[4] Muslim (67).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taaliki ya ”Fitnat-ut-Takfiyr”, uk. 24-25
  • Imechapishwa: 18/10/2021