Ni kipi kinachosemwa wakati mtu anapochemua au kwenda miayo?


Swali: Je, ipo du´aa maalum ya kusoma wakati anapochemua au anapokwenda miayo?

Jibu: Hapana. Mtu anapochemua au kwenda miayo hakuna du´aa ya kusoma, tofauti na wanavyofikiria wasiokuwa na elimu. Watu wasiokuwa na elimu wanapochemua husema ”Alhamdulillaah”. Himdi zote njema zinamwendea Allaah juu ya kila hali, lakini hakuna dalili yoyote kwamba amuhimidi Allaah baada ya kupia miayo.

Vivyo hivyo wanapopiga miayo husema:

أعوذ بالله من الشيطان الرجيم

“Najilinda kwa Allaah kutokamana na shaytwaan aliyefukuzwa mbali.”

Hili halina msingi. Hakuna dalili kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alikuwa anafanya hivo.

Pengine mtu akauliza kama kwenda miayo sio neema kutoka kwa Allaah na kwamba mtu anatakiwa kumuhimidi Allaah juu ya neema. Hapana shaka yoyote kwamba ni neema, lakini bado hakuna dalili kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akimuhimidi Allaah wakati anapokwenda miayo. Kwa hivyo kitendo hicho hakikuwekwa katika Shari´ah. Kwa sababu wanazuoni wanao kanuni inayotambulika inayosema kwamba kila kitu ambacho ilipatikana sababu yake wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hakuifanya, basi kufanywa kwake sio Sunnah. Kitendo cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Sunnah, na kule kuacha kwake pia ni Sunnah. Kupiga miayo kulikuwepo wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wala yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwa akimuhimidi Allaah kwayo, kwa hiyo kuacha kuhimidi ndio Sunnah.

Vivyo hivyo kuomba ulinzi kwa Allaah dhidi ya shaytwaan aliyefukuzwa mbali baada ya kupiga miayo. Pengine mtu akasema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Kupiga miayo kunatokana na shaytwaan.”

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ ۚ إِنَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

“Pindi utakapokuchochea uchochezi kutokana na shaytwaan, basi taka ulinzi kwa Allaah. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mjuzi wa kila kitu.”[1]

Lakini makusudio ya maneno Yake (Ta´ala):

وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ ۚ إِنَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

“Pindi utakapokuchochea uchochezi kutokana na shaytwaan, basi taka ulinzi kwa Allaah. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mjuzi wa kila kitu.”

ni kwamba pale unapoazimia kutenda dhambi au kuacha jambo la wajibu, basi hapo unatakiwa kumtaka hifadhi Allaah. Shaytwaan ndiye mwenye kuamrisha kufanya maovu:

الشَّيْطَانُ يَعِدُكُمُ الْفَقْرَ وَيَأْمُرُكُم بِالْفَحْشَاءِ

“Shaytwaan anakutishieni ufukara na anakuamrisheni machafu.”[2]

Kunapotokea jambo hili, basi mtakeni ulinzi Allaah. Lakini inapokuja katika kupiga miayo, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kupiga miayo kunatokana na shaytwaan. Pindi anapopiga miayo mmoja wenu basi azuie kwa kiasi anavyoweza. Pindi mmoja wenu anapopiga miayo shaytwaan humcheka.”

Hakusema mtu amtake ulinzi Allaah pindi anapokwenda miayo. Hiyo ikajulisha kwamba kumtaka ulinzi Allaah dhidi ya shaytwaan aliyewekwa mbali wakati mtu anapokwenda miayo sio Sunnah.

[1] 07:200

[2] 02:268

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa' al-Baab al-Maftuuh (22 A) Tid:25:44
  • Imechapishwa: 18/08/2021