Ni ipi hukumu ya msafiri kufunga pamoja na kwamba ana uzito?

Swali 403: Ni ipi hukumu ya msafiri kufunga pamoja na kwamba ana uzito?

Jibu: Ikiwa kufunga kunamtia uzito usiyokuwa na uhakika basi imechukizwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona mwanaume ambaye amefanyiwa kivuli na watu wamemsongamana ambapo akasema:

“Huyu ana nini?” Wakasema: “Amefunga.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Si katika wema kufunga safarini.”[1]

Ama kama anahisi uzito mkubwa basi ni italazimika kwake kuacha kufunga. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikula wakati aliposhtakiwa na watu kwamba swawm imekuwa ngumu kwao. Kisha akaelezwa kwamba wapo ambao wameendelea kufunga ambapo akasema:

“Hao ndio waasi. Hao ndio waasi.”[2]

Ama kuhusu yule ambaye swawm si ngumu kwake basi bora ni yeye kufunga kwa sababu ya kumuigiza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa vile alikuwa akifunga. Abu Dardaa´ (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Tulikuwa pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Ramadhaan katika joto kali. Hakuna miongoni mwetu aliyekuwa amefunga isipokuwa tu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ´Abdullaah bin Rawaahah.”[3]

[1] al-Bukhaariy (1946) na Muslim (1115).

[2] Muslim (1114).

[3] al-Bukhaariy (1945) na Muslim (1122).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Arkaan-il-Islaam, uk. 462
  • Imechapishwa: 06/05/2019