Ni ipi hukumu ya kutundika hirizi?


Swali: Ni ipi hukumu ya kutundika hirizi?

Jibu: Kutundika hirizi na kinga kumegawanyika sehemu mbili:

Ya kwanza: Kile kilichotundikwa kiwe ni katika Qur-aan. Wanachuoni wa kale na wa sasa wametofautiana katika hilo. Kuna waliojuzisha hilo na kuonelea kuwa linaingia katika maneno Yake (Ta´ala):

وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ

“Tunateremsha katika Qur-aan ambayo ni shifaa na rehema kwa waumini.” (17:82)

كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ

“Kitabu Tumekiteremsha kwako kikiwa ni chenye baraka.” (38:24)

 Wakasema miongoni mwa baraka zake ni kuining´iniza ili izuie mabaya.

Kuna wengine wamekataza hilo na wakasema kuitundika ni jambo halijathibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba ni sababu iliyowekwa katika Shari´ah ambayo inazuia au kuondosha ovu. Wamesema kuwa msingi katika mambo kama haya ni kukomeka (Tawqiyf). Haya ndio maoni yenye nguvu na kwamba haijuzu kutundika hirizi hata kama itakuwa ni katika Qur-aan tukufu. Haijuzu vilevile kuiweka chini ya mto wa mgonjwa, kuitundika ukutani na mfano wa hayo. Kinachotakiwa ni kumsomea mgonjwa na kumuombea du´aa moja kwa moja. Hivyo ndivyo alivyokuwa akifanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Ya pili: Kile kilichotundikwa kikawa sio Qur-aan tukufu miongoni mwa vitu visivyofahamika maana yake. Haijuzu kwa hali yoyote. Kwa sababu haijulikani ni kipi kilichoandikwa. Baadhi ya watu huandika talasimu na mambo yaliyo funganafungana ambayo ni herufi zilizoingilianaingiliana unazokaribia kutozielewa na kuzisoma. Haya ni katika Bid´ah na ni haramu. Hayajuzu kwa hali yoyote.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (01/106-107)
  • Imechapishwa: 10/06/2017