Ni ipi hukumu ya kusherehekea siku ya mama?


Swali: Ni ipi hukumu ya kusherehekea yale yanayoitwa ´siku ya mama`?

Jibu: Sikukuu zote zinazopingana na Shari´ah zote ni sikukuu za ki-Bid´ah na zilizozuliwa ambazo zilikuwa hazitambuliki wakati wa as-Salaf as-Swaalih. Pengine ikawa vilevile waliozianzisha ni wasiokuwa waislamu. Katika hali hiyo pamoja na kuwa ni Bid´ah inakuwa ni kujifananisha na maadui wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Sikukuu zilizowekwa katika Shari´ah zinatambulika kwa waislamu. Nazo ni ´Iyd-ul-Fitwr, ´Iyd-ul-Adhwhaa na sikukuu ya wiki ambayo ni siku ya ijumaa. Katika Uislamu hakuna sikukuu mbali na hizi tatu. Sikukuu nyengine zote zilizozuliwa mbali na hizo ni zenye kurudishwa kwa yule mwenye nazo na ni batili katika Shari´ah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo atarudishiwa.”

Bi maana atarudishiwa mwenyewe na si yenye kukubaliwa mbele ya Allaah. Katika matamshi mengine imekuja:

“Atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu atarudishiwa.”

Hayo yakibainika basi sikukuu hiyo inayoitwa ´sikukuu ya mama` itakuwa haijuzu. Haijuzu kuzua kitu katika nembo za sikukuu kama mtu kudhihirisha furaha, kutoa zawadi na mfano wa hayo.

Lililo la wajibu kwa muislamu ni yeye kujitukuza na kujifakharisha na Uislamu wake na atosheke na yale aliyoyawekea mpaka Allaah (Ta´ala) na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika dini hii iliyonyooka ambayo Allaah (Ta´ala) amewaridhia waja Wake. Asizidishe na wala asipunguze ndani yake.

Kinachotakiwa kwa muislamu vilevile asiwe kipofu mwenye kufuata kila mwenye kubwabwaja. Bali inapaswa utu wake uwe kwa mujibu wa Shari´ah ya Allaah (Ta´ala) ili awe mwenye kufuatwa na si mwenye kufuata, kuigizwa na si mwenye kuigiza. Kwa sababu Shari´ah ya Allaah imekamilika kwa njia zote. Allaah (Ta´ala) amesema:

الْيَوْمَ يَئِسَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن دِينِكُمْ فَلَا تَخْشَوْهُمْ وَاخْشَوْنِ ۚ الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

“Leo Nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni Uislamu uwe dini yenu.” (05:03)

Allaah ana haki zaidi kuliko kumfanyia sherehe siku moja tu kwa mwaka. Bali mama ana haki kwa mwanae amlinde, amtilie umuhimu na asimame kwa kumtii katika yasiyokuwa kumuasi Allaah (´Azza wa Jall). Haya yanatendeka katika kila zama na pahali.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (03/302)
  • Imechapishwa: 09/06/2017