Ni ipi hukumu ya Kumtakia rehema al-Wasswaabiy?


Kuna kijana mmoja ameuliza swali. Ninachelea ya kwamba ameyasikia kutoka kwa mtu ambaye ni mkubwa. Aliniuliza ninavyoonelea juu ya kumtakia rehema Shaykh fulani. Nilijibu kwa ugumu kidogo na kusema:

“Karibuni badala yake nitakutakia rehema wewe.”

Hivi kweli mwanafunzi anaweza kuuliza swali kama hili? Inafaa likazunguka kati ya wanafunzi? Baada ya kumnasihi kijana huyu nikapata khabari ya kwamba wagonjwa wamejaza intaneti kwa hadithi hizi. Watu hawa wanawashawishi wanachuoni na kusababisha magomvi kati yao. Wao sio wanachuoni, hawana elimu yoyote. Allaah amrehemu mtu mwenye kujua kadri ya nafsi yake. Kumbe ameandika kwenye intaneti:

“Allaah amewasalimisha waislamu na mzushi huyu.”

Wanamaanisha mwanachuoni huyu aliyefariki; Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab al-Wasswaabiy (Rahimahu Allaah). Ni katika wanachuoni bora kabisa wa Yemen. Watu wote wanamjua. Wanachuoni wanamjua; Shaykh Ibn Baaz, Shaykh Ibn ´Uthaymiyn, Muftiy na Shaykh Swaalih al-Fawzaan. Wote hawa wanamjua ni nani. Kila mtu anajua kuwa ni katika wanachuoni bora kabisa wa Salafiyyuun na katika wanachuoni bora kabisa wa Yemen. Ni mmoja katika wanachuoni wa Shaykh Muqbil (Rahimahu Allaah). Ninasema kuwaambia hawa wenye papara ya kuwahukumu waislamu wengine na khaswa wanachuoni:

Nyama za wanachuoni ni zenye sumu

ni jambo linalojulikana nini Allaah anachowafanya wale wenye kuwaponda

Mcheni Allaah kutokana na wanachuoni. Mcheni Allaah (´Azza wa Jall):

مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ

“Hatamki kauli yeyote isipokuwa yuko karibu naye mwangalizi amejitayarisha [kurekodi].” (50:18)

Kuna watu wenye kudai kuwa na elimu kazi yao ni kujishughulisha na kuleta ugomvi kati ya wanachuoni. Wamemgawa na kumfanyia Tabdiy´ huyu na yule, wamemfanyia Tafsiyq na kumkufurisha huyu na yule – pasi na kumwogopa Allaah wala aibu. Haya yanatokamana na kwamba wanafikiri kuwa wanaweza. Ni mtihani wao. Ni jambo la khatari kabisa mtu kufikiri kuwa anaweza na kudai elimu. Ni jambo ambalo wamejaribiwa kwalo watu wengi hii leo. Mshairi amesema:

Kinachonitia kinyaa na Andalusia

ni majina kama Mu´tadhwid na Mu´tamid

majina makubwa kwa watu wasiyoyastahiki

kama mfano wa paka anayejipigia makofi

inapoiga mashambulizi ya simba

Ninaomba kinga kwa Allaah kutokana na upungukiwaji baada ya ukamilifu. Ninamuomba Allaah kinga kutokamana na fitina. Hii ni fitina. Baadhi ya watu wamepewa mtihani kwa kufikiri kuwa wana elimu na kupenda umaarufu. Wanachotaka ni kuonekana. Wanachotaka ni kuitwa “´Aalim”, “´Allaamah” au “Shaykh”. Wamehadaika na majina haya. Hivi mabarabaro wanastahiki kuitwa “´Allaamah” na “Shaykh”? Hata wanachuoni wakubwa hawaitwi hivyo. Leo vijana wanaitwa hivyo. Mcheni Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Zihifadhini ndimi zenu na khaswa inapokuja katika kuwaponda wanachuoni. Ni jambo la khatari. Zingatieni Kauli ya Allaah (Ta´ala):

وَقِفُوهُمْ ۖ إِنَّهُم مَّسْئُولُونَ

“Wasimamisheni, hakika wataulizwa.” (37:24)

مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ

“Hatamki kauli yeyote isipokuwa yuko karibu naye mwangalizi amejitayarisha [kurekodi].”

وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا

“Na wala usiyafuate [kusema au kufanya] yale usiyokuwa nayo elimu. Hakika masikio na macho na moyo; vyote hivyo vitaulizwa.” (17:36)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hifadhi huu.”

Bi maana ulimi.

“Mtu anaweza kutamka neno asilolipa uzito wowote na matokeo yake likamtupa kwenye Moto wa miaka sabini.”

“Hivi mnamjua ni nani mfilisikaji?” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Mfilisikaji ni yule asiyekuwa na chochote.” Akasema: “Mfilisikaji ni yule ambaye atakuja siku ya Qiyaamah na swawm, swalah na zakaah hali ya kuwa amemtukana huyu, amemtuhumu huyu na amemdhulumu huyu. Hivyo huyu na yule wachukue kutoka kwenye matendo yake mema. Yatapoisha matendo yake mema kabla ya kupata hukumu yake kwa ajili ya madambi yake, yatachukuliwa madhambi yao na kupewa yeye. Hatimaye atupwe Motoni.” (Muslim (2581)).

Nyinyi wenye kuwagawa watu hivi kweli hamumchi Allaah! Hamumchi Allaah? Nyinyi wenye kuwajeruhi watu bila ya dalili hivi kweli hamumchi Allaah! Hamumchi Allaah? Nyinyi ambao mmejiweka katika ngazi za kina Yahyaa bin Ma´iyn, Imaam Ahmad na Shu´bah bin Hajjaaj! Hamumchi Allaah? Allaah amrehemu mtu ambaye anajua kadri ya nafsi yake. Mcheni Allaah (´Azza wa Jall) na zihifadhini ndimi zenu isije kufeli na kuwaponda wanachuoni.

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin Sa´d as-Suhaymiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://olamayemen.com/Dars-14798
  • Imechapishwa: 13/09/2020