Ni ipi hukumu ya kumchelewesha maiti mpaka ndugu zake wafike?

Swali: Ni ipi hukumu ya kuchelewesha kuliswalia jeneza mpaka wahudhurie ndugu wa maiti na ni kipi kidhibiti juu ya hilo?

Jibu: Kuchelewesha kumwandaa maiti na kumswalia ni kwenda kinyume na Sunnah na ni kwenda kinyume na yale aliyoamrisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

“Lifanyisheni haraka jeneza. Endapo atakuwa ni mtu wa kheri, basi itakuwa ni kheri inayomtangulizia. Akiwa ni kinyume na hivyo, itakuwa ni shari mnayojitwisha kwenye mabega yenu.”

Haifai kuwasubiri. Isipokuwa ikiwa ni kwa muda mdogo kama mfano wa saa moja au saa mbili. Ama kulichelewesha kwa muda mrefu ni jambo linaenda kinyume na Sunnah. Vilevile ni kumfanyia jinai maiti. Nafsi njema pindi watu wa maiti wanapomtoa huwaomba wamuharakishe. Hili ni kwa kuwa ameahidiwa kheri na thawabu kubwa1.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/77)
  • Imechapishwa: 17/06/2017