Ni ipi hukumu ya kukausha viungo vya wudhuu´?

Swali: Ni ipi hukumu ya kukausha viungo vya wudhuu´?

Jibu: Kukausha viungo vya wudhuu´ haina neno. Msingi ni kwamba hakuna neno. Kwa sababu msingi ni kutokuwepo kizuizi. Msingi katika mikataba na matendo – mbali na mambo ya ´ibaadah – ni kuruhusu mpaka kupatikane dalili inayokataza. Pengine mtu akauliza ni vipi tutajibu Hadiyth ya Maymuunah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesimulia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitawadha halafu akampelekea leso ambapo akairudisha na akaanza kuyakung´uta maji kwa mkono wake. Jibu ni kwamba kitendo hichi cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni qadhiya maalum ambayo inaweza kuwa na tafsiri nyingi: ima ni kutokana na sababu fulani kwenye leso ile, haikuwa safi, anachelea isije kulowa kwa maji, japokuwa sababu hii si ya sawa. Kwa hivyo kunaweza kuwa na tafsiri nyingi. Lakini hata hivyo kule kuletewa kwake leso inawezekana ikawa ni dalili inayofahamisha kuwa ilikuwa ni katika mazowea yake kukausha viungo vya mwili. Vinginevyo asingemletea.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/153)
  • Imechapishwa: 02/07/2017