Ni ipi hukumu ya kubadilisha rangi ya mvi?

Swali: Ni ipi hukumu ya kuzibadilisha ndevu, masharubu na mvi za kichwani kwa kuzitia rangi? Ikiwa ni Sunnah ni kwa nini tunawaona wanachuoni wengi hawafanyi hivo[1]?

Jibu: Kuzitia mvi rangi, mbali na rangi nyeusi, ni Sunnah iliyoamrishwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Zibadilisheni mvi hizi na jiepusheni [na rangi] nyeusi.”

Lakini wanachuoni wengi hawafanyi hivo kutokana na uzito wa kuliendea hilo. Mtu anatakiwa kuwa makini na nywele zake. Vinginevyo mashina yake yataonekana na kufichuka. Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema kuhusu kuzitia rangi nywele za kichwani:

“Ni Sunnah. Iwapo tungelikuwa na nguvu kwalo tungelitendea kazi. Lakini hata hivyo lina uzito na ugumu.”

Akaliacha kutokana na ugumu na uzito. Huu ndio udhuru wa baadhi ya wanachuoni ambao hawafanyi hivo.

Mwaliu wetu ´Abdur-Rahmaan as-Sa´diy (Rahimahu Allaah) ndevu alikuwa hazipaki kitu. Muftiy wa nchi hii Shaykh Muhammad bin Ibraahiym (Rahimahu Allaah) alikuwa hazitii rangi mvi zake. Vivyo hivyo ndugu zake wengine na wanachuoni wengi tuliokutana nao hawatii rangi yoyote. Lakini hata hivyo ni Sunnah na imethibiti. Hili halina shaka. Ni mamoja inatendewa kazi na wanachuoni au haitendewi kazi na wanachuoni. Inatakiwa kwa mtu kuzibadilisha rangi mvi zake. Lakini hata hivyo aepuke rangi nyeusi. Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“… na jiepusheni [na rangi] nyeusi.”

[1] Tazama https://firqatunnajia.com/ni-ipi-hukumu-ya-kutia-rangi-ndevu-kwa-hina-au-katam/

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (30)
  • Imechapishwa: 23/10/2017