Ni ipi hukumu ya ambaye anasawazisha ndevu zake zilingane?

Swali: Ni ipi hukumu ya ambaye anasawazisha ndevu zake zilingane?

Jibu: Lililo la wajibu ni kurefusha ndevu, kuziacha na kuzifuga na kuzishambulia kwa chochote. Hilo ni kutokana na yale yaliyothibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

”Fupisheni masharubu na refusheni ndevu. Jitofautisheni na washirikina.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah) pia amepokea katika ”as-Swahiyh” yake kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Fupisheni masharubu na refusheni ndevu. Jitofautisheni na washirikina.”

Muslim vilevile amepokea katika ”as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Punguzeni masharubu na refusheni ndevu. Jitofautisheni na washirikina.”

Hadiyth zote hizi zinafahamisha juu ya ulazima wa kurefusha, kuacha na kufuga ndevu na ulazima wa kupunguza masharubu. Hili ndio jambo lililowekwa katika Shari´ah na ndio jambo la lazima ambalo ameelekeza na akaliamrisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kufanya hivo ni kumwigiliza yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kujitofautisha na washirikina. Vilevile ni kujitenga mbali na kujifananisha nao na kujifananisha na wanawake.

Kuhusu yale aliyopokea at-Tirmidhiy (Rahimahu Allaah) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba alikuwa akikata ndevu zake urefu na upana wake, wanachuoni wanaona kuwa hizi ni khabari batili. Hazikusihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wamezishikilia baadhi ya watu ilihali ni khabari ambazo hazikusihi. Kwa sababu katika cheni ya wapokezi wake kuna bwana mmoja anaitwa ´Umar bin Haaruun al-Balkhiy ambaye ametuhumiwa uongo. Kwa hiyo haijuzu kwa muumini kushikilia Hadiyth hii batili na wala kuchukua ruhusa kwa yale yanayosemwa na baadhi ya wanachuoni. Sunnah ndio yenye kuhukumu na amuzi juu ya kila mmoja. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ

“Atakayemtii Mtume, basi kwa hakika amemtii Allaah.”[1]

قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ ۖ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْهِ مَا حُمِّلَ وَعَلَيْكُم مَّا حُمِّلْتُمْ ۖ وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا ۚ وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ

”Sema: ”Mtiini Allaah na mtiini Mtume, mkigeukilia basi hakika jukumu lake ni lile alilobebeshwa nanyi ni juu yenu yale mliyobebeshwa; na mkimtii mtaongoka na hapana juu ya Mtume isipokuwa ufikishaji wa wazi.”[2]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi; mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[3]

[1] 04:80

[2] 24:54

[3] 04:59

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/443)
  • Imechapishwa: 10/12/2020