Nguzo za Uislamu ni tano peke yake


Swali: Nimewasikia baadhi ya wanachuoni wakizingatia kuwa kuamrisha mema na kukataza maovu ni nguzo miongoni mwa nguzo za Uislamu. Je, ni sahihi?

Jibu: Ndio, yamesemwa na baadhi ya wanachuoni. Lakini hata hivyo hakujapokelewa dalili ya wazi juu ya hilo. Si vinginevyo ni moja katika faradhi kubwa katika Uislamu. Nguzo za Uislamu ambazo amezibainisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahuu ´alayhi wa sallam) ni tano. Amesema (Swalla Allaahuu ´alayhi wa sallam):

”Uislamu umejengwa juu ya vitano; kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Namna hii ndivo Mtume (Swalla Allaahuu ´alayhi wa sallam) alibainisha nguzo na misingi ya Uislamu. Kwa hivyo haijuzu kuzidisha juu yake isipokuwa kwa dalili ambayo ni sahihi.

Lakini kuamrisha mema na kukataza maovu ni msingi miongoni mwa misingi na ni faradhi miongoni mwa faradhi. Lakini haisemwi kuwa ni nguzo ya sita kwa sababu hakuna dalili ya hilo. Ni kama ambavo kupambana katika njia ya Allaah ni msingi miongoni mwa mambo ya misingi. Vivyo hivyo kujiepusha na mambo ya haramu ambayo Allaah amewaharamishia waja Wake ni msingi wa lazima miongoni mwa misingi ya lazima. Lakini hata hivyo hakusemwi kuwa ni nguzo miongoni mwa nguzo za Uisamu kwa kutokuweko dalili ya hilo. Pamoja na kutambua kwamba tunalazimika kunyooka juu ya yale yote ambayo Allaah amewajibisha na tujiepushe na yale yote aliyoharamisha Allaah.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (05/74)
  • Imechapishwa: 24/01/2021