1 Mwenyezi Mungu asema:

“Nilikuwa tayari kujionesha

kwao wasiouliza habari zangu.

Nilikuwa tayari kuwapokea

wale wasionitafuta.

Nililiambia taifa ambalo halikuomba kwa jina langu:

”Nipo hapa! Nipo hapa!”

2 Mchana kutwa niliwanyoshea mikono watu waasi,

watu ambao hufuata njia zisizo sawa,

watu ambao hufuata fikira zao wenyewe.

3Ni watu ambao daima hunichokoza waziwazi;

hutambikia miungu yao katika bustani,

na kuifukizia ubani juu ya matofali.

4Huketi makaburini na kukaa mafichoni usiku.

Hula nyama ya nguruwe na mchuzi wa wanyama haramu.

5Huwaambia wale wanaokutana nao:

“Kaeni mbali nami;

msinikaribie kwani mimi ni mtakatifu!”

Watu hao wananikasirisha mno,

hasira yangu ni kama moto usiozimika.

6“Jueni kuwa nimelitia jambo hilo moyoni,

sitanyamaza bali nitawafanya walipe;

nitawafanya walipe kwa wingi.

7Mimi Mwenyezi Mungu, nitawalipiza maovu yao

wayalipie na maovu ya wazee wao.

Wao waliifukizia ubani miungu yao milimani,

wakanitukana mimi huko vilimani.

Nitawafanya walipe kwa wingi,

watayalipia matendo yao ya awali.”

  • Marejeo: Isaya 65:01-07 https://www.bible.com/sw/bible/74/ISA.65.BHN
  • Imechapishwa: 02/02/2020