Ndoto hutokea kama inavyosimuliwa

120- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Ndoto hutokea kama inavyoelezwa. Mfano wa hilo ni kama mtu aliyenyanyua unyayo wake na anasubiri ni lini atautua chini. Mmoja wenu akiona ndoto asimweleze isipokuwa mtoaji nasaha au msomi.”

Ameipokea al-Haakim (4/391) kupitia ´Abdur-Razzaaq: Ma´mar ametuhadithia, kutoka kwa Ayyuub, kutoka kwa Abu Qilaabah, kutoka kwa Anas, kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema:

”Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.”

adh-Dhahabiy ameafikiana naye. Walikuwa na haki ya kuongeza kwamba imeafikiana na masharti ya al-Bukhaariy…

Kwa hiyo Hadiyth ni Swahiyh.

Hadiyth ni dalili ya wazi kwamba ndoto hutokea kama inavyosimuliwa. Ndio maana Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatueleza mtu asimweleze yeyote isipokuwa mtoa nasaha au ambaye ni msomi. Kwa sababu makusudio ni kwamba wote wawili wanatakiwa kuichagulia maana nzuri kabisa ili ije kutokea kama ilivyoelezwa. Lakini hata hivyo inatakiwa ndoto hiyo iwe inawezekana kuelezwa kwa njia hiyo, japokuwa ni kwa mtazamo mmoja, na isiwe ni kosa kabisa. Vinginevyo itakuwa haina taathira yoyote na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (1/1/239)
  • Imechapishwa: 27/04/2019