Ndio maana ´Umar alikuwa akichapa

3173- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Umefanya vizuri Ibn-ul-Khattwaab.”

Ameipokea Ahmad: Muhammad bin Ja´far ametuhadithia: Shu´bah ametuhadithia, kutoka kwa al-Azraq bin Qays, kutoka kwa ´Abdullaah bin Rabaah, kutoka kwa mmoja katika Mswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumaliza kuswali ´Aswr, alisimama bwana mmoja kuswali. Wakati ´Umar alipomuona akachukua nguo au kanzu yake na akasema: “Keti chini. Hakika si vyenginevyo kilichowaangamiza watu wa Kitabu ni kwamba hakukuwa na kipambanuzi kati ya swalah zao.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Umefanya vizuri Ibn-ul-Khattwaab.”

Abu Ya´laa pia ameipokea katika “al-Musnad” yake. Cheni ya wapokezi ni Swahiyh na wapokezi wote ni waaminifu kwa mujibu wa sharti za Muslim. Isipokuwa Swahabah ambaye hakutajwa jina, lakini hata hivyo haidhuru, kwa sababu Maswahabah wote ni waadilifu.

Mtu akiuliza ni vipi itasihi kutumia Hadiyth hii ya kukubali kwa ´Umar ilihali ni jambo limesihi kwamba alikuwa akiwapiga wale wenye kuswali Rak´ah mbili baada ya ´Aswr, jibu ni kwamba kuwapiga kwake ilikuwa kwa lengo la kuziba njia na kuchelea kwake hatimaye wasije kuswali katika kipindi ambacho jua limeshapiga manjano. Hayo ndio makusudio ya zile Hadiyth zote zinazokataza moja kwa moja kuswali baada ya ´Aswr, na si kwamba haijuzu kuziswali Rak´ah mbili hizo kabla jua halijapiga manjano. Kwa ajili hiyo ndio maana hakumkataza bwana huyo kuswali moja kwa moja baada ya ´Aswr. Kinachotilia nguvu hilo ni kwamba as-Saa-ib amesema juu ya Zayd bin Khaalid al-Juhaniy:

“Khaliyfah ´Umar bin al-Khattwaab alimuona akiswali Rak´ah mbili baada ya ´Aswr ambapo akampiga bakora. Alipomaliza kuswali akamwambia: “Ee kiongozi wa waumini, unachapa! Sintoacha kuziswali baada ya kumuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaziswali.” ´Umar akasema: “Ee Zayd! Nisingechapa watu kwazo kama ingekuwa si kuchelea watu wakaja kuswali mpaka usiku.”

Alichokuwa anamaanisha ´Umar ni kule kuchelea mtu kuziswali wakati jua liko lazama, jambo ambalo linaafikiana na maneno yaliotangulia ya mwanae.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (7/1/525-526)
  • Imechapishwa: 11/08/2020