Nasaha za Rabiy´ al-Madkhaliy juu ya mtu kuitafuta haki kokote ilipo na kutokuwa na ushabiki kwa walinganizi waliokosolewa

Ninawausia watoto na ndugu zangu kuitafuta haki na kuitafiti katika kila jambo miongoni mwa mambo. Ni mamoja jambo hilo iwe katika yale yaliyoafikiana kwayo au katika yale waliyotofautiana kwayo.

Muumini anayeukusudia uso wa Allaah na Pepo nafsi yake hairidhiki isipokuwa mpaka pale atapoifikia haki. Hili khaswa linahusiana na yale mambo ya tofauti na kipindi cha wakati wa fitina. Hatikisiki hata mara moja isipokuwa kwa mujibu wa haki, elimu na umaizi.

Watu wawili wakitofautiana – hata kama atakuwa ni baba yake au mwalimu wake – basi haijuzu kwake kusimama upande wake au dhidi yake isipokuwa mpaka baada ya kuyadurusu mambo hayo na kuyatambua ukweli wake kikamilifu. Baada ya hapo ndipo anachukua msimamo wake na anasimama upande wa haki iliyombainikia. Hili ndilo la wajibu kwa muislamu. Vinginevyo ni katika mienendo ya kipindi kabla ya kuja Uislamu na ushabiki wa batili wa kipindi kabla ya kuja Uislamu. Haimstahikii muislamu na wala haijuzu akapita juu ya mfumo huu muovu.

Wana wetu na ndugu zetu! Nakuusieni kumcha Allaah na kwa yale niliyoyataja. Mnatakiwa kuipenda haki. Mnatakiwa kuitafuta haki mahala kokote ilipo mpaka kufikia katika ukweli.

Nawausia wana na ndugu zangu kuuheshimu mfumo wa Salaf, kuwa na uthabiti juu yake na kuwaheshimu wanachuoni wake pindi wanapoisema haki. Katika hali hiyo haijuzu kupingana nao.

Wakizungumzia suala fulani na wakalitolea dalili, basi hana yeyote udhuru wa kupingana nao. Vilevile haijuzu kwa yeyote kukinzana nao. Haya ni matendo ya Ahl-ul-Ahwaa´ wanaojaribu kuuangusha mfumo wa Salaf na wanachuoni wake.

Inapokuja katika Jarh na Ta´diyl, basi inatosha kule Jarh kuwa imetoka kwa mwanachuoni mmoja kama ambavyo vilevile inatosha kule Ta´diyl kuwa imetoka kwa mwanachuoni mmoja. Hii ina maana ya kwamba wanachuoni wawili ambao wote ni wakweli, wanaokubalika na waliosalimika kutokamana na matamanio wakitofautiana juu ya mtu fulani, basi lililo la wajibu kwa wanachuoni wengine wamuombe dalili yule mwanachuoni mkosoaji. Akitoa dalili, basi ni wajibu kwao kujisalimisha na dalili na hoja hizi. Endapo yule msifiaji au mwengine atayapuuza – kuzirudisha dalili – basi papo hapo uadilifu wake unaanguka. Kuanzia hapo atakuwa haaminiwi juu ya dini ya Allaah. Ikiwa mwanachuoni mmoja ataleta hoja na dalili za kutosha na akapingwa na makumi ya wanachuoni wengine kwa batili, uongo na kwa vitimbi, asiwaachie nafasi. Hii ni moja katika kanuni za Jarh na Ta´diyl ambayo inatulazimu katika mfano wa fitina kama hizi.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://subulsalam.com/play.php?catsmktba=27615
  • Imechapishwa: 03/04/2017