Swali: Mvutaji sigara anaguswa na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kuiua nafsi yake yuko Motoni.”

Au Hadiyth ilio na maana kama hiyo. Je, mvutaji sigara anaingia katika haya? Ni zipi nasaha zako kwa wale ndugu zetu waliopewa mtihani huu?

Jibu: Mvutaji sigara hapana shaka kwamba ameiweka nafsi yake khatarini. Madaktari wote wameafikiana juu ya kwamba sigara ina madhara na kwamba ni sababu inayopelekea kupatwa na kansa ya kooni na mapafuni. Madhara yake yako wazi. Watazame wale waliopewa mtihani nayo utawaona wakiwa ni wenye hamu duni na matashi dhaifu. Pale wanapopunguza unawaona wakiwa wachangamfu na nguvu.

Ni jambo linalotambulika kwamba huenda wakawepo watu ambao hawadhuriki nayo kwa hali yoyote. Kwa sababu tunawaona watu ambao wanaitumia pamoja na hivyo wana afya. Lakini mwishowe ni lazima imdhuru. Endapo wangejiepusha nayo wangelikuwa na nguvu zaidi na afya njema.

Kwa ajili hiyo tunasema kuwaambia wale waliopewa mtihani wa sigara wamuombe Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) awaepushe nayo, warudi kwa Allaah na amtake msaada Yeye kuiacha na aiache pole pole. Vilevile anatakiwa kuwaepuka wale wanaoitumia ili wasimuingize kwa mara nyingine. Allaah anapotaka kumkinga mtu basi humpa maazimio yenye nguvu kabisa. Hakika sisi tumewaona watu walio na maazimio ambapo wakawa wameiacha kabisa na hawakurudi tena. Lakini tatizo ni kwamba watu wengi maazimio ya ni dhaifu. Utawaona vifua vyao vinaingiwa na dhiki na wanarudi kuvuta ambapo wanashindwa kuvumilia. Lakini endapo wangesubiri na kustahamili basi Allaah angeliwasalimisha.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (41) http://binothaimeen.net/content/1586
  • Imechapishwa: 17/10/2018