Nasaha kwa wale wanaokesha usiku na kushinda mchana wamelala Ramadhaan

Swali: Unawanasihi nini wale wanaotumia muda mwingi wa mchana wa Ramadhaan kulala na kufanya Dhikr kwa uchache? Tunaomba uwaelekeze watu hawa katika kitendo sahihi na Allaah akujaze kheri.

Jibu: Mimi nawaelekeza ndugu zangu wote, nikianza na nafsi yangu, ya kwamba tutumie fursa ya mwezi huu uliobarikiwa – namuomba Allaah atufikishe sisi na nyinyi hali ya kuwa ni wenye kufunga na wenye kusimama kwa ajili ya kuswali, wenye kufunga hali ya kutarajia malipo kutoka Kwake. Tuutumie kwa kufanya matendo mema katika Dhikr, kisomo cha Qur-aan, swalah, swadaqah, kuwatendea wema wazazi wawili, kuwaunga ndugu na tabia njema. Kwa sababu ni mwezi ambao huenda usirudi kwa mtu mara nyingine.

Kuhusu wale wanaokesha usiku na wanashinda wamelala mchana ni katika watu waliokhasirika zaidi. Kwa sababu wameupoteza usiku katika mambo yasiyokuwa na faida ndani yake. Bali huenda ndani yake kuna madhara. Vilevile wameupoteza mchana wao kwa kulala sana. Huenda hata wakalala na kupitwa na swalah ya Dhuhr na ´Aswr.

Nasaha zangu kwa ndugu zangu waislamu wamche Allaah (´Azza wa Jall) na watumie fursa hii ya msimu. Kwani, hakika naapa kwa Allaah, ni kubwa zaidi kuliko msimu wa kuuza na kununua katika uwajibu wa kuupupia.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (70) http://binothaimeen.net/content/1597
  • Imechapishwa: 18/03/2020